Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Taifa Stars mambo yazidi kuwa magumu AFCON

Msuva Mnsz Taifa Stars mambo yazidi kuwa magumu AFCON

Mon, 22 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kundi F la fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka huu zinazoendelea huko Ivory Coast limezidi kuwa gumu baada ya timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Zambia.

Matokeo hayo yamefanya timu nne zilizopo katika kundi hilo, Morocco, DR Congo, Zambia na Taifa Stars kila moja kuwa na nafasi ya kufuzu hatua ya 16 bora kutegemeana na matokeo ya mechi za mwisho zitakazochezwa Januari 24.

Ingawa Taifa Stars inashika mkia katika kundi hilo na pointi yake moja, inaweza kufuzu hatua ya 16 bora ikiwa itaibuka na ushindi katika mechi ya mwisho dhidi ya DR Congo na Zambia ikashindwa kupata ushindi dhidi ya Morocco.

Lakini hata Zambia ikishinda, Taifa Stars inaweza kufuzu ikiwa itaifunga DR Congo kupitia nafasi nne zinazotolewa kwa timu zilizoshika nafasi ya tatu zikiwa na matokeo bora kwenye makundi.

Kwa sasa Morocco inaongoza kundi F ikiwa na pointi nne, ikifuatiwa na DR Congo na Zambia ambazo kila moja ina pointi mbili na Taifa Stars iko mkiani ikiwa na pointi moja.

Bao la Taifa Stars katika mchezo huo lilifungwa na Simon Msuva dakika ya 12 baada ya kupokea pasi kutoka kwa nahodha, Mbwana Samatta huku lile la Zambia likifungwa na Patson Daka dakika ya 88 akiunganisha kwa kichwa kona ya Clatous Chama.

Kwa upande mwingine, bao la Msuva lilimfanya amfikie Mbwana Samatta katika chati ya wafungaji bora wa muda wote wa Taifa Stars likiwa la 22.

Lakini pia limemfanya Msuva abakishe mabao matatu tu ili aifikie rekodi ya Mrisho Ngassa ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Taifa Stars akiwa na mabao 25.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live