Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Taifa Stars katikati ya mtego

Taifa Stars Players Kikosi cha Taifa Stars

Mon, 17 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Taifa Stars ina kibarua kizito mbele ya Morocco na Zambia katika kinyang'anyiro cha kupigania nafasi ya kushiriki Finali za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika kwa mara ya kwanza kwenye mataifa ya Marekani, Mexico na Canada.

Katika makundi tisa ya timu sita sita, Taifa Stars imepangwa kundi E pamoja na vigogo hivyo, huku timu nyingine zikiwa Congo, Niger na Eritrea.

Kinyang'anyiro hicho kitaanza kutimua vumbi kuanzia Novemba 13, 2023 hadi Oktoba 14, 2025. Washindi wa kila kundi watafuzu moja kwa moja kwenye fainali hizo huku timu nne bora zilizoshika nafasi ya pili, zitachuana kwenye mchujo, merchi zitakazochezwa kati ya Novemba 10-18, 2025.

Taifa Stars itakuwa na michezo 10 katika hatua hiyo ya makundi, mitano itakuwa nyumbani huku mingine ikiwa ugenini, bado ratiba haijapangwa lakini mchezo wa kwanza na wa pili itakuwa kati ya 13-21 Novemba wa tatu na nne kati ya 3–11 Juni 2024, wa tano hadi sita ni kati ya 17–25 Machi 2025. Mchezo wa saba hadi nane kati ya 1–9 Septemba 2025, wa tisa na kumi ni kati ya 6–14 Octoba 2025.

Kiujumla hawa ndio wapinzani wa Taifa Stars na ubora wao kwenye viwango vya FIFA na mienendo yao kwa miaka ya hivi karibuni hapo chini ni namna ambavyo Tanzania ilivyo kwenye mtego inaopaswa kuutegua kabla ya kuzipigia fainali hizo za 23 za Dunia tangu ilipoanza 1930.

KAZI IPO HAPA

Tanzania haijawahi kushiriki fainali za Kombe la Dunia tangu michuano hiyo ilipoasisiwa mwak 1930, zaidi ya kushiriki mechi za mchujo za barani Afrika na kuishia njiani.

Rekodi zinaonyesha miaka miwili tofauti 1978 na 1994 Tanzania ilijitoa kwenye mechi za mchujo, huku mingine ikishindwa kushiriki mchujo kwa kutolewa awali au kuishia hatua ya makundi kwa michuano ya CAF na kuziacha timu nyingine zikienda kuliwakilisha bara hilo la Afrika.

Mwaka 1978 Stars ilijitoa raundi ya kwanza ya mechi za mchujo ilipokuwa imepangwa kuvaana na Uganda kutokana na sababu za kisiasa kwani kipindi hicho ndipo kulipokuwa na vuguvugu la Vita vya Kagera vilivyoziingiza nchi nchi katika vita kali iliyomalizika 1979.

Mara ya pili kwa Tanzania kujitoa ilikuwa 1994 katika mechi za makundi ikiwa katikati na safari hii itakuwa na kazi ya kukomaa ili angalau kuwa miongoni mwa timu tisa zitakazoiwakilisha Afrika au hata kuangukia kwenye ile play off ya timu nne washindwa bora zitakzochuana hatua hiyo.

Kocha Adel Amrouche aliyeteuliwa hivi karibuni wakati Stars ikipambana kusaka tiketi za Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 zitakazofanyika mwakani nchini Ivory Coast na kutoka patupu anapaswa kujipanga mapema na jeshi atakalounda ili kundika rekodi mpya.

Kocha huyo aliyewahi kuinoa Harambee Stars ya Kenya atakuwa na kazi ya kufuata nyayo za makocha wenzake wa kigeni waliowahi kuivusha Taifa Stars kwenye fainali kubwa zikiwamo za Afcon 1980 na 2019 pamoja na zile za Chan 2009 na 2020 kwa kuipeleka Tanzania fainali za Dunia.

Tanzania ilifuzu fainali za Afcon 1980 zilipofanyikia Nigeria ikiwa na kocha Mpoland, Slawomir Wolk aliyesaidiwa na Paul West Gwivaha na Joel Bendera, kisha mwaka 2019 Mnigeria Emmanuel Amunike aliipeleka fainali za Afcon zilizofanyika Misri.

Mbrazili Marcio Maximo aliyeipeleka Tanzania kwenye Fainali za Kombe la Mataifa kwa Wachezaji wa Ndani (Chan) za mwaka 2009 zilipofanyikia Ivory Coast, kisha Etienne Ndayiragije wa Burundi akaivusha Stara katika fainali za Chan 2020 zilizofanyikia Cameroon.

Hata hivyo, ni lazima ajipange kwelikweli kwa mechi hizo 10 za kundi hilo la E kama kweli inataka kupenya kutokana na ukweli wapinzani wake sio wa mchezo mchezo, hasa inapokuja michuano mikubwa kama hiyo ambayo safari hii imeongeza idadi ya timu shiriki kwa Afrika kutoka watano hadi tisa na mwingine wa ziada.

MOROCCO

Timu ya taifa ya Morocco ilianzishwa mwaka 1928 na ilicheza mchezo wake wa kwanza Disemba 22 mwaka huo dhidi ya timu B ya Ufaransa, ambayo ilipoteza kwa mabao 2-1.

Hili ni moja ya taifa lenye nguvu kwenye soka la Afrika na mwaka jana, 2022 kwenye Fainali zilizopita za Kombe la Dunia kule Qatar tuliona walivyoweka rekodi ya kufika hatua ya nusu fainali.

Miamba hii ambayo mwaka 1976 ilitwaa ubingwa wa Afcon na kushika nafasi ya pili 2004 inashika nafasi ya 13 kwenye viwango vya ubora wa soka Duniani vitolewavyo na FIFA, nafasi ya juu zaidi kwao ni 10 ambayo walishika April 1998.

Taifa Stars ambayo nafasi ya juu zaidi kwenye viwango vya FIFA ni 65 na ilikuwa Februari 1995 itakuwa na kibarua cha kufanya kutokana na ubora wa Morocco ambao nyota wake wengi wamekuwa wakifanya vizuri kwenye klabu mbalimbali kubwa barani Ulaya.

Mwaka 2013, Taifa Stars ilicheza dhidi ya Morocco kuwania kufuzu Kombe la Dunia, ilivuna pointi tatu ikiwa nyumbani kwa ushindi wa mabao 3-1 na kupoteza tatu ikiwa ugenini kwa mabao 2-1.

ZAMBIA

Msiba mzito uliwahi kuikumba timu ya Zambia wakati ndege ya kijeshi (REG: AF-319) iliyokuwa ikisafirisha timu kwenda Senegal kwa mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia la FIFA 1994 ilipoanguka jioni ya Aprili 27, 1993.

Hawa ni majirani zetu hawapo mbali na ukanda wa Afrika Mashariki, ni taifa la mpira na linahistoria ya kutwaa fainali za mataifa wa Afrika, walifanya hivyo 2012 nchini Gabon. Tangu hapo wakapotea kwenye soka la ushindani.

Chipolopolo wapo nafasi ya 84 kwenye ubora wa viwango vya FIFA wamepanda kwa nafasi mbili, nafasi yao ya juu kabisa kwenye viwango hivyo ni 15 na ilikuwa Februari – Mai 1996, Agosti 1996.

Tanzania haina rekodi nzuri dhidi ya Zambia, mataifa hayo yamekutana mara 32 katika mashindano mbalimbali ikiwemo michezo ya kirafiki, Taifa Stars imeshinda mara tano tu, sare tisa na kupoteza mara 18 dhidi ya Chipolopolo.

Katika michezo mitatu iliyopita Taifa Stars imepoteza mfululizo dhidi ya Chipolopolo, mara ya mwisho ilikuwa kwenye mchezo wa CHAN Januari 19, 2021, ilikumbana na kichapo cha mabao 2-0.

CONGO Timu ya taifa ya Congo ilicheza mechi yake ya kwanza Februari 1960 ilikuwa ya kujipima ubavu dhidi ya Ivory Coast ambayo walipoteza kwa mabao 4-2.

Wapo nafasi ya 106 kwenye viwango vya FIFA, ukiziondoa Morocco na Zambia hawa ndio wanaoonekana wababe kwenye kundi E kwa kuangalia orodha ya ubora wa viwango iliyotolewa Juni 29 mwaka huu, 2023.

Nafasi ya juu zaidi kwao kwenye viwango vya FIFA ni 42 (Septemba 2015). Wanaijua vizuri Tanzania hivyo maandalizi kwa Taifa Stars yanatakiwa kuwa sawasawa kutokana na ubora wao.

NIGER

Ingawa ni moja wapo ya timu zisizo na mafanikio katika ukanda wa Afrika Magharibi wenye nguvu, Niger imekuea na mienendo kadhaa mizuri katika mashindano ya kufuzu.

Moja ya matokeo yao bora zaidi ilikuwa katika mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia la FIFA la 1982 ambapo Niger iliondoa Somalia na Togo kwa sheria ya bao la ugenini, lakini wakafungwa na Algeria katika raundi ya tatu ambapo ni timu nane pekee zilizosalia.

Niger imeshuka kwa nafasi tano kwenye viwango vya FIFA kwa sasa wapo nafasi ya 128, waliwahi kuwa nafasi ya 68 ilikuwa Novemba 1994, nafasi mbovu zaidi kwao ilikuwa 196 (Agosti 2002)

Mara ya mwisho kwa Niger kucheza dhidi ya Taifa Stars ilikuwa Juni 18 mwaka huu kwenye uwanja wa Benjamini Mkapa, bao la Simon Msuva lilitosha kuwapa raha Watanzania kwenye mchezo huo wa kuwania nafasi ya Fainali za Mataifa ya Afrika.

ERITREA

Timu ya Eritrea ilishiriki katika mashindano ya kirafiki nchini Sudan mwaka wa 1992, mwaka mmoja kabla ya Eritrea kupata uhuru.

Eritrea ilishiriki Kombe la CECAFA la 1994, lililoandaliwa na Baraza la Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati, ingawa ENFF haikuanzishwa hadi 1996.

Timu ya kwanza kamili ya kimataifa ilikuwa katika Kombe la CECAFA la 1999, mwaka mmoja baada ya ENFF kujiunga na CAF na FIFA.

Hawa ndio vibonde ambao wanatazamwa pengine na kile timu kwenye kundi, wanashika nafasi ya 198 kwenye viwango vya FIFA nafasi ya juu zaidi kwao ni 121 na ilikuwa Agosti 2007.

Taifa Stars haijapoteza hata mara moja kwenye michezo minne waliyokutana dhidi ya Eritrea michezo yote ikiwa kwenye michuano ya CECAFA, ilishinda mara tatu na kutoka sare mara moja.

Chanzo: Mwanaspoti