Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Taifa Stars ilee makundi

74845 Stars+pic

Mon, 9 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Taifa Stars imetinga katika hatua ya makundi ya kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika Qatar 2022 baada ya kuiondosha Burundi kwa ‘matuta’, shukrani kwa ushujaa wa kipa Juma Kaseja.

Stars inaungana na timu nyingine 13 zilizopita katika hatua ya awali ya mchujo na kuungana na mataifa 26 yanayoongoza katika viwango vya soka Afrika kufanya timu 40 zitakazochuana katika hatua ya makundi ya kuwania kufuzu.

Makundi 10 ya timu nne-nne yatapangwa na mshindi wa kila kundi ndiye atakayeingia katika hatua ya mwisho ya mchujo, ambapo kila mmoja atapangiwa mpinzani wake mmoja kucheza mechi mbili (nyumbani na ugenini) na timu zitakazopita zitaenda kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar 2022.

Kwenye Uwanja wa Taifa jana, baada ya dakika 120 na sare ya 1-1, mechi iliingia hatua ya kupigiana penalti kwa vile matokeo ya awali ugenini Burundi pia yalikuwa bao 1-1.

Licha ya presha kubwa ya hatua ‘matuta’, Watanzania waliweka matumaini kwa kipa wao mkongwe Juma Kaseja ambaye katika maisha yake ya soka amejenga heshima kubwa kwa uwezo wake wa kuokoa penalti.

Na hakuwaangusha Watanzania baada ya kufuta penalti ya kwanza ya Warundi, ambao penalti zao nyingine walipiga nje ya lango ikiwamo wa nahodha wao, Saido Berahino.

Pia Soma

Advertisement
Erasto Nyoni, Himid Mao na Gadiel Michael walifunga penalti zote tatu za Taifa Stars na hapakuwa na haja ya wageni kupiga penalti yao ya nne baada ya kukosa zote tatu za kwanza.

Stars ilipata goli la kuongoza katika dakika ya 29 kupitia kwa nahodha Mbwana Samatta akitumia vyema kona iliyochongwa na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.

Baada ya kuingia bao hilo, kasi ya Stars ilionekana kupungua tofauti na ilivyokuwa dakika za mwanzo za mchezo jambo lililowapa mwanya Burundi kurudi mchezoni na kuanza kupishana na wenyeji hao.

Makosa ya safu ya ulinzi ya Stars katika kuwadhibiti washambuliaji wa Burundi, yaliwazawadia bao la kusawazisha wapinzani wao dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza.

Bao hilo lilifungwa na Fiston ambaye pamoja na wenzake wawili walikuwa huru kufanya wanachotaka ndani ya boksi baada ya mabeki wa Stars kuparaganyika.

Sare hiyo ya bao 1-1 ilidumu hadi mwamuzi Norman Matemera kutoka Zimbabwe alipopuliza kipyenga cha kuashiria mapumziko.

Katika kipindi hicho cha kwanza, Kessy alionyeshwa kadi ya njano kwa kumchezea faulo, Amissi.

Wachezaji wa Stars mara mbili walimlalamikia mwamuzi Matemera ikiwa ni madai ya penalti moja likiwa ni lile la dakika ya 11 ambapo Dilunga aliangushwa na Nsabiyumva na mwamuzi huyo kuamua kona na mara ya pili ilikuwa ni kupitia shambulizi la Msuva ambapo ilionekana kama beki Nshimihirimana David amenawa ndani ya eneo la hatari.

Stars waliingia kipindi cha pili wakiwa na kasi kama ile waliyoanza nayo kipindi cha kwanza lakini bado utulivu safu ya ushambuliaji ilikuwa ni tatizo kutokana na nafasi zilizokuwa zikipotea.

Dakika ya 60, ilionekana kama Nshihirimana amenawa mpira wakati alipokuwa kwenye jitihada za kuokoa krosi ya Tshabalala lakini licha ya malalamiko ya wachezaji wa Stars, mwamuzi aliamuru kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Katika dakika ya 61, Stars ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Dilunga nafasi yake ilichukuliwa na Farid Musa. Stars waliendelea kushambulia zaidi kupitia pembeni mwa uwanja lakini idadi kubwa ya krosi walizopiga ziliokolewa na walinzi wa Burundi.

Kutokana na majeraha ya beki wao Racanamwo Joel, Burundi walilazimika kumfanyia mabadiliko dakika ya 66 nafasi yake ilichukuliwa na Ngando Omar ambapo dakika mbili baadaye nahodha wao Berahino alionyeshwa kadi ya njano kwa kumfanyia madhambi Kessy.

Stars ilifanya mabadiliko ya mwisho dakika ya 70 na 72 kwa kuwatoa Tshabalala na Abubakar Salum nafasi zao zilichukuliwa na Gadiel Michael na Shaban Chilunda.

Kwa upande wa Burundi, dakika ya 78 walimtoa Fiston aliyeumia na nafasi yake ilichukuliwa na Bimenyimana Caleb huku dakika ya 86 walimtoa Kanakimana na kumuingiza Shasir Nahimana.

Stars waliendelea kumiliki mpira na kutengeneza idadi kubwa ya nafasi na mashambulizi ya mara kwa mara ambayo hayakuzaa mabao.

Kwa upande wa Burundi wenyewe waliamua kucheza kwa kutumia mbinu ya kufanya mashambulizi ya kustukiza langoni mwa Stars ambayo yalionekana tishio mno kwa wenyeji.

Miongoni mwa mashambulizi hayo ni lile la dakika ya 89 ambapo Shasir alimtengea pasi nzuri Caleb ambaye alipiga shuti lililookolewa kwa ustadi na Juma Kaseja aliyeupangulia mpira juu ya goli na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda. Licha ya mwamuzi wa mezani Brighton Chimene kutoka Zimbabwe kuongeza dakika nne, mechi hiyo ilimalizika kwa sare hiyo ya bao 1-1 na hivyo kulazimika mechi hiyo kwenda dakika 30 zanyongeza ili kumpata mshindi kufuatia timu hizo mechi ya kwanza kumalizika kwa sare kama hiyo jijini Bujumbura.

Stars

Juma Kaseja, Hassan Kessy, Mohamed Hussein/ Gadiel Michael, Kelvin Yondani, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Iddi Selemani, Abubakar Salum, Mbwana Samatta/ Himid Mao, Saimon Msuva, Hassan Dilunga/ Farid Musa.

Burundi

Ndikumana Justin, Diamanti Ramazani, Racanamwo Joel, Nsabiyumva Fredric, Nshihirimana David, Bigirimana Gael, Amissi Cedric, Kanakimana Bienvenu, Berahino Saido, Abdulrazack Fiston, Amissi Mohamed

Chanzo: mwananchi.co.tz