Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Taifa Stars hakuna namna

Taifa Starssss Taifa Stars hakuna namna

Sun, 18 Jun 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Hakuna namna zaidi ya ushindi. Ndivyo hesabu zilivyo kwa timu ya taifa, Taifa Stars wakati leo jioni itakapoikaribisha Niger katika mechi ya raundi ya tano ya Kundi F kuwania tiketi ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon), 2023 zitakazofanyika mwakani kule Ivory Coast.

Stars iliyopoteza mchezo uliopita ikiwa nyumbani dhidi ya Uganda ambayo Saa 12:00 jioni itakuwa wenyeji wa vinara wa kundi hilo, Algeria inahitaji ushindi wa aina yoyote ili kujiweka salama kwenye mbio za kwenda kwenye fainali za tatu katika historia ya Tanzania kwenye michuano hiyo ya Afcon.

Tanzania ilishirika mara ya kwanza fainali hizo mwaka 1980 zilipofanyikia Nigeria na kukaa kwa miaka 39 kabla ya kufuzu tena mwaka 2019 na katika msimamo kwa sasa Stars ipo nafasi ya piliikiwa na pointi nne kama ilivyo kwa Uganda iliyopo nafasi ya tatu, huku Algeria iliyokwishakata tiketi ya Ivory ikiwa kileleni na pointi 12 wakati Niger inaburuza mkia na alama mbili tu.

Wachezaji 25 walioingia kambini mapema mwanzoni mwa wiki kabla ya kutangazwa na Kocha Amrouche walikuwa wakijifua kwa ajili ya mchezo huo muhimu kabla ya kusaliwa na mechi ya kufungia michuano hiyo itakapocheza ugenini dhidi ya Algeria Septemba 4 mwaka huu.

Nahodha Mbwana Samatta sambamba na mastaa wengine kama Bakar Mwamnyeto, Dickson Job, Himid Mao, Adi Yusuf, Mzamiru Yassin, Mohammed Hussein 'Tshabalala', Kibu Denis, John Tiber, Abdi Banda na wengineo wana kazi kubwa ya kuzitumia dakika 90 Kwa Mkapa kuibeba Stars.

Matokeo ya aina yoyote ya kupoteza kwa mechi hiyo ya nyumbani, huku Uganda ikpata matokeo mazuri mbele yas Algeria inaweza kufifisha safari ya Tanzania kwenda Ivory Coast, kwani mechi ya ugenini na Algeria inaweza kuwa ngumu kulingana na rekodi zilizopo baina ya timu hiyo mjini Algers.

Kocha Amrouche na nahodha, Mbwana Samatta wamewaahidi Watanzania ushindi kwa kujua huo ni mchezo muhimu kwa Stars na wa mwisho wa nyumbani kutokana na maandalizi iliyofanya kwa siku ambazo timu ilikuwa kambini kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

"Haitakuwa kazi rahisi, lakini tumejiandaa kuwapa raha mashabiki kwani huu ni mchezo wa mwisho nyumbani kwenye michuano hii na unahotajika kushinda kuweka hai matumaini ya kwenda Afcon 2023, naomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kuisapoti timu yetu," alisema Amrouche.

KAZI IPO

Katika mechi za msimu huu wa kusaka tiketi hiyo ya Afcon 2023, Stars haijapata ushindi nyumbani, kwani ilianza kwa kuchapwa mabao 2-0 na Algeria kisha kulala 1-0 mbele ya Uganda, mara baada ya kutoka kushinda ugenini 1-0 dhidi ya The Cranes.

Stars kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Niger uliopigwa Juni mwaka jana iliambulia sare ugenini kwa bao la dakika ya kwanza tu la George Mpole ambaye safari hii hakuitwa kikosini kabla ya wenyeji kuchomoa dakika ya 26 kupitia Daniel Sosah mwenye mabao mawili hadi sasa katika michuano hiyo.

Kutokana na rekodi mbovu ya nyumbani, Stars leo inahitaji ushindi ili kutuliza roho za mashabiki wa soka ambao wamepunguza mzuka kutokana na matokeo ya mchezo uliopita dhidi ya Uganda ambao licha ya ahamasa kubwa kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan na viiongozi wengine kununua tiketi na kuruhusu mashabiki kuingia bure uwanjani, haikusaidia kwa kulala 1-0 na kutibua hesabu.

Kwa namna mchezo huo ulivyo na umuhimu mkubwa, kocha Amrouche anapaswa kushuka uwanjani leo akiwa na kikosi kitakachompa matokeo ili kusikilizia baadae matokeo ya Uganda na Algeria kabla ya kuifuata Algeria, Septemba 4 kujua kama itaenda Ivory Coast au itakuwa 'asante na kwaheri'.

Kocha huyo anahitajika kuwatumia wachezaji wenye kasi kubwa na watakozitumia nafasi watakazozitengeneza, sambamba na kuwazuia Waniger kutopata mwanya wa kumtungua iwe ni Beno Kakolanya au Metacha Mnata atakayeanza langoni mwa Stars.

Niger ni timu inayoshambulia kupitia pembeni na inayomtegemea sana Sosah, mbali na kuwepo kwa wakali wengine kama Victorien Adebayor, Amadou Moutari na Amodou Wonkoye, bila kusahau viungo Abdoul Soumana na nahodha Youssouf Oumarou.

Hata hivyo uwepo kwa kina Abdi Banda, beki mzoefu sambamba na Mwamnyeto, Ibrahim Bacca ndani ya Stars pamoja na kina Samatta, Msuva, Abdul Suleiman 'Sopu', viungo wa kazi, Himid Mao, Mzamiru, Novatus Dismas na wakali wengine, matumaini ya Stars ni makubwa kwa leo.

WAAMUZI

Mechi hiyo itakayoanza saa 10:00 jioni itachezeshwa na waamuzi kutoka Misri, atakayepuliza kipyenga pale kati atakuwa ni, Mohamed Al Sayd, akisaidiwa na Youssef Elbosaty na Samy Halhal, huku mezani atakuwepo Mahmoud Nagi.

Bingwa mtetezi wa Afcon kwa sasa ni Senegal iliyotwaa msimu uliopita kwa kuifunga Misri kwa penalti 4-2 baada ya dakika 120 kumalizika kwa suluhu, huku mfungaji bora alikuwa ni Vincent Aboubakar wa Cameroon aliyemaliza na mabao manane.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live