Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Taifa Stars: Waleteni hao Morocco

Samatta Hakimu Taifa Stars: Waleteni hao Morocco

Wed, 17 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Umewahi kusikia stori ya sisimizi kumuangusha tembo? Ndivyo ambavyo wachezaji wa Taifa Stars wanaamini inawezekana kupambana na kupata matokeo mazuri Jumatano ya Januari 17 dhidi ya Morocco kwenye mchezo wao wa kwanza wa Fainali za Matifa ya Afrika.

Taifa Stars ambayo inashiriki kwa mara ya tatu fainali hizo, itacheza mchezo wake huo wa kwanza katika kundi F kwenye uwanja wa Laurent Pokou huko San Pedro, Ivory Coast. Uwanja huo una uwezo wa kuingiza watazamaji wapatao 20,000.   Simon Msuva ni miongoni mwa wachezaji hao ambaye alisema anaiheshimu Morocco kutokana na ukubwa wao kwenye soka la Afrika na hata duniani kwa ujumla lakini hilo haliwafanyi kukwamisha mipango waliyonayo dhidi yao.

“Morali ya timu ni kubwa sana, tumekuwa tukijiandaa hatua kwa hatua, hatupo hapa kushiriki, tupo kwa ajili ya kushindana na lolote linaweza kutokea, sisi kama wachezaji hakuna timu ambayo tunaihofia,” alisema.

Kwa upande wake, Haji Mnoga ambaye hii itakuwa mara yake ya kwanza kucheza fainali hizo kubwa zaidi Afrika, alisema,

“Hii ni ndoto yetu na lazima wachezaji tujitoa kwa ajili ya Watanzania ambao wapo nyuma yetu, tunakazi kubwa ya kufanya na tupo tayari kwa ajili ya taifa letu.”

Mara baada ya kumalizana na Morocco, kituo kinachofuata kwa vijana hao wa Adel Amrouche ni kucheza dhidi ya Zambia, Jumapili ya Januari 21 kisha kumalizana na DR Congo, Jumatano ya Januari 24  kwenye hatua ya makundi.

Hii ni mara ya tatu kwa Tanzania kushiriki fainali za Afcon baada ya awali kuzicheza za mwaka 1980 zilipofanyikia Nigeria na 2019 ilienda Misri, huku matumaini ya Watanzania yakiwa kwa kocha Adel Amrouche anayeinoa timu hiyo akisaidiana na Hemed Suleiman ‘Morocco’ na Juma Mgunda.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live