MANCHESTER, ENGLAND. OLE Gunnar Solskjaer ataambia watu nini. Manchester United imekumbana na vichapo vitatu katika mechi nne za mwisho, presha inazidi kumpanda kocha huyo.
Kocha huyo raia wa Norwayr hajabeba taji lolote tangu apewe mikoba ya kuinoa timu hiyo mwishoni mwa 2019, lakini dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi amewaongeza Cristiano Ronaldo, Jadon Sancho na Raphael Varane kwenye kikosi.
Lakini, vichapo kutoka kwa Young Boys, West Ham na Aston Villa katika michuano mitatu tofauti vimeanza kuibua maswali mengi kama Solskjaer ni mtu sahihi wa kuendelea kuinoa timu hiyo.
Shabiki wa Man United na mwandishi Scott Paterson, anayeandikia Republik of Mancunia, tovuti ya mashabiki wa miamba hiyo ya Old Trafford ameweka wazi mtazamo wa mashabiki juu ya Solskjaer.
Mashabiki hawapingi kwamba timu imepoteza mechi tatu kati ya nne - tena kwenye michuano tofauti. Wasiwasi wao ni kwa kocha Solskjaer kama ni mtu sahihi katika kuwafikisha hatua ya juu zaidi.
Msimu uliopita aliifikisha timu fainali ya Europa League, lakini ikapoteza kwa mikwaju ya penalti mbele ya Villarreal.
Msimu huu kuna mabadiliko makubwa yamefanyika. Mabosi wamempa sapoti kunasa wachezaji wenye uwezo wa kuifanya timu kupiga hatua ya juu zaidi na hatimaye kubeba mataji. Lakini, hivi unavyosoma hapa, tayari imeshapoteza taji moja baada ya kutupwa nje kwenye Kombe la Ligi na West Ham.
Kwenye Ligi Kuu England, kuwa nyuma kwa tofauti ya pointi moja na vinara ni nafasi nzuri ukilinganisha na msimu uliopita hali ilivyokuwa baada ya mechi sita za awali.
Timu bado inashikilia rekodi ya kutopoteza ugenini kwenye Ligi Kuu England, hilo linaleta tofauti. Kuna sababu ya mechi walizochapwa kwa msimu huu. Aaron Wan-Bissaka alionyeshwa kadi nyekundu ikiwa imebaki saa zima kwenye mechi dhidi ya Young Boys na Cristiano Ronaldo alinyimwa penalti dhahiri kabla ya makosa ya dakika za mwisho ya Jesse Lingard yaliyowapa nafasi wapinzani wao kufunga bao.
Dhidi ya West Ham, Lingard alilalamika apewe penalti na mwamuzi, Jon Moss aligoma licha ya kutazama tukio hilo kwa umakini kabisa na kuonekana Mark Noble alimvuta Lingard na kumwangusha ndani ya boksi.
Kisha kichapo cha wikiendi iliyopita, 1-0 dhidi ya Aston Villa, straika Ollie Watkins alimzuia kipa David de Gea jambo ambalo alipaswa kuwa ameotea kabla ya Kortney Hause kufunga kwa kichwa kuwapa Aston Villa pointi tatu muhimu uwanjani Old Trafford, huku Man United ikipoteza mastaa wawili - Harry Maguire na Luke Shaw kwa majeraha.
Mambo yangesawazishwa, lakini Bruno Fernandes alibadili staili ya upigaji penalti na kukosa mkwaju dakika za majeruhi, kitu kilicholizamisha jahazi la Man United na kushindwa walau kupata pointi moja kwenye mechi hiyo.
Staili iliyozoeleka ya Bruno kupiga penalti ni ile anarudi nyuma, anatulia, anatisha anaruka na kupiga mpira, lakini wikiendi iliyopita akitulia tu na kupiga mpira ambao ulipaa.
Mashabiki wa Man United wanamgeukia Solskjaer. Kwanza wanamwona anavifuja tu, havitumii ipasavyo vipaji vilivyopo kwenye kikosi.
Wanachokiona kwa kocha huyo kwamba amezidisha tu nguvu ya kulialia kwa waamuzi kwamba wanamnyima ushindi.
Mashabiki wanaamini kwamba kama Solskjaer angekuwa na mfumo mzuri wa kuwachezesha wachezaji wake, kusingekuwa na visingizio kwa waamuzi kwamba wamemnyima ushindi. Solskjaer anapaswa kujitathmini.
Man United ilimiliki mpira kwa asilimia 60 dhidi ya West Ham ya David Moyes kwenye Kombe la Ligi. Ilipiga mashuti kadhaa, lakini hakuna lililokwenda kwenye nyavu.
Dhidi ya Aston Villa ilimiliki mpira kwa asilimia 60 na kupiga mashuti kibao, lakini hakukuwa na bao.
Leo, Jumatano Man United itakipiga na Villarreal. Itakuwa mechi ya tatu kwa mashabiki wa timu hiyo kuishuhudia uwanjani Old Trafford ndani ya wiki moja, lakini wasiwasi umekuwa mkubwa. Man United haikupangwa na wapinzani wagumu sana kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, tofauti na msimu uliopita ilipowekwa kwenye Kundi la Kifo, hivyo kwa msimu huu Solskjaer hana cha kujitetea timu ikishindwa kuvuka hatua ya makundi.
Anaweza kutaka kufanya mabadiliko ya kikosi chake cha kwanza, hasa baada ya Maguire na Shaw kuwa majeruhi, lakini hapaswi kufanya mabadiliko ya kikosi kizima. Uamuzi wowote atakaofanya basi ulenge kuhakikisha timu inapata matokeo dhidi ya timu inayoshika nafasi ya 11 kwenye msimamo La Liga.
Jadon Sancho anapaswa kupewa nafasi ya kuanza, wakati Solskjaer akimpendelea Mason Greenwood upande wa wingi ya kulia, huku mashabiki wakihoji inakuwaje mchezaji ambaye alisumbuka kumsajili, kisha hamchezeshi na kumwaacha benchi. Haipingwi kwamba Greenwood amekuwa akifanya mambo makubwa kwenye kikosi, lakini hilo halina maana ya kumweka benchi Sancho. Mashabiki wanamtaka Solskjaer atafute namna ya kuwatumia wachezaji wote hao wawili.
Nahodha wa zamani wa miamba hiyo ya Old Trafford, Gary Neville alidai kwamba amekuwa akiitazama Man United ya sasa kama timu ya uwezo binafsi wa mchezaji mmoja mmoja, wakisubiri tu kuonyesha makali makubwa kwenye mechi kubwa na si timu yenye mtiririko wa kucheza kitimu na kushinda mechi.
“Kama hakuna mbinu, hakuna mzuka,” alisema Neville akijaribu kupaza sauti ya mashabiki kwa kocha Solskjaer, licha ya kukubali kwamba amekuwa akijaribu kuiboresha timu hiyo kwenye msimamo wa ligi kwa kila msimu. Mambo yanatajwa kuwa mazuri kwenye vyombo vya kubadilishia, lakini shida inakosekana uwanjani, Man United imekuwa haina muunganiko, hivyo inashindwa kucheza kwa kiwango bora cha kuwapa ushindi.
Mashabiki wanachosema ni kwamba kama anatokea mchezaji mwenyewe tu anapambana kuisaidia timu kushinda, hapo Solskjaer hatastahili kupewa pongezi. Kama anapongezwa, basi hata anaposhindwa kurekebisha kikosi mchezaji mmoja anapotolewa kwa kadi nyekundu, kutoa uamuzi sahihi wa mchezaji gani apige penalti au ni aina gani ya mtindo ya uchezaji unaopaswa, basi lazima zote zitakuwa zinamhusu.
Man United ina wachezaji, tena wenye vipaji vikubwa kwelikweli. Solskjaer anahitaji kuwatumia wachezaji wake bora kabisa kupata matokeo.
Kama unakuwa safu ya ulinzi yenye mabeki mahiri kama Raphael Varane na Maguire, kwanini Solskjaer amekuwa akiendelea kuwatumia Fred na Scott McTominay kwa pamoja kufanya kazi ya kukaba. Mashabiki wanachosema ni kwamba sawa staili hiyo inaweza kutumika kwenye mechi dhidi ya timu ngumu kama Chelsea, Manchester City na Liverpool, lakini si kwa timu nyingine za kawaida kama Aston Villa.
Marcus Rashford si muda mrefu atarejea uwanjani baada ya kukosakana kwa zaidi ya miezi minne. Kurejea kwake kutakitikisa kikosi cha Man United. Kwenye hilo, kuwa na timu itakayokuwa na uwezo mkubwa wa kushambulia na kuwa na wafungaji wa mabao wengi ndani ya uwanja, Solskjaer anapaswa kuachana na mtindo wake wa kuendelea kuwatumia viungo wawili wa kukaba, McTominay na Fred kwenye timu yenye mabeki Maguire na Varane.
Anapaswa kuwa na chaguo moja tu la kiungo mkabaji kwenye timu ambayo ukuta wake una wachezaji wote makini, kuanzia golini kwa David De Gea, kulia kwa Aaron Wan-Bissaka na kushoto kwa Luke Shaw.
Kurudi kwa Rashford bila shaka kumfanye aanze kwenye upande wa kushoto. Hapo, Pogba atalazimika kurudi kiungo ya kati akicheza na mmoja kati ya Fred, McTominay au Nemanja Matic. Upande wa kulia, Sancho na Greenwood watakuwa na kazi ya kupigania nafasi na kwenye straika wa kati ibaki kuwa vita ya Cristiano Ronaldo na Edinson Cavani. Ukweli ni kwamba ni ngumu kwa Solskjaer kutafuta kisingizio cha timu kufanya vibaya kutokana na vipaji vikubwa vilivyopo kwenye timu. Man United yenye Pogba, Bruno Fernandes, Ronaldo na Cavani haipaswi kutaabika kufunga mabao.
Solskjaer asipochanga karata na kuifanya iendelee kucheza soka linalolingana na homa za vipindi - kupanda na kushuka hatakuwa na usalama wa kutosha kuhusu ajira yake.
Msimu huu kumaliza bila taji lolote hakuwezi kumsaidia kibarua chake kitaota mbawa. Mei bado mbali, lakini kila kitu kinaanzia sasa. Anapaswa kutoa nafasi kwa wachezaji bora na si kupanga kikosi kwa woga, kupanga viungo wawili wa kukaba hata mechi dhidi ya West Ham United.