Tabora United Jana Jumapili Februari 25 imeshindwa kufurukuta nyumbani baada ya kubanwa na kutoka sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mbele ya Singida Fountain Gate katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.
Wenyeji imelazimika kusubiri dakika saba kabla ya pambano hilo kumalizika kuchomoa bao lililowekwa kimiani kwa kichwa na Mganda John Ben Nakibinge baada ya awali beki Yahya Mbegu wa Singida kuwafungia wageni bao dakika ya 53.
Matokeo hayo yameifanya Tabora kufikisha pointi 18 na kupanda kwa nafasi moja kutoka 13 hadi ya 12 ikilingana na Kagera Sugar ambayo itakuwa uwanjani kuvaana na Ihefu katika mechi itakayopigwa Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Kwa upande wa Singida matokeo hayo yameifanya ifikishe pointi 21 ikiwa nafasi ya saba na ikiwa ni pointi ya kwanza kwa timu hiyo tangu Ligi Kuu irejee kutoka kwenye mapumziko ya kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 na Fainali za Afcon 2024 zilizomalizika hivi karibuni huko Ivory Coast.
Singida ilishushwa na Namungo iliyolazimishwa sare ya 2-2 na KMC kwenye Uwanja wa Azam Complex, jijini Dar es Salaam katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyoingia raundi ya 17 kwa sasa.
Katika mechi hiyo ya jana wenyeji ilitangulia kupata mabao kupiotia Raheem Shomary na Daruwesh Saliboko kabkla ya wageni kuchomoa kupitia Meddie Kagere na Ibrahim Mkoko.
Ligi hiyo itaendelea tena keshokutwa Jumanne kwa KMC kuwa wageni wa JKT Tanzania mechi itakayopigwa saa 1:00 usiku, mara baada ya pambano kati ya vibonde Mtibwa Sugar itakayoialika Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Manungu.
Yanga ndio inayoendelea kuongoza msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 43 kupitia mechi 16, huku Mtibwa ikiwa mkiani na pointi nane tu baada ya kushuka uwanjani mara 16 pia.