Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tabora Utd wafichua kinachoendelea kambini

Tabora United Www Tabora Utd wafichua kinachoendelea kambini

Thu, 15 Feb 2024 Chanzo: Dar24

Uongozi wa Tabora United umesema timu yao haikufanya vyema katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na kukumbwa na upepo mbaya, huku wakiweka wazi hawana changamoto ya ukata ndani ya timu hiyo.

Ofisa Habari wa Tabora United, Christina Mwagala, amesema kufanya vibaya kwa timu yao hakuhusiani na suala la madai kwa wachezaji, ukata wa kulipa mishahara, badala yake ni bahati mbaya tu, lakini wana imani watafanya vizuri mzunguko wa lala salama.

“Hatuna changamoto yoyote kama wachezaji wanadai mishahara inachelewa, hapana wachezaji wetu wanalipwa mishahara kwa wakati, wanalipwa tarehe 23, ikichelewa tarehe 25 kwa hiyo matokeo haya hawawezi kuhusishwa na vitu kama hivyo, hayahusiani, ni upepo mbaya tu umetukumba,” amesema Mwagala.

Amewataka mashabiki wa soka Tabora kuiunga mkono na kuahidi kuanza kufanya vizuri katika mechi za mzunguko wa pili.

“Niwasihi sana mashabiki wa klabu ya Tabora United tushikamane, tuwe kitu kimoja, tuwasapoti vijana wetu, naamini mzunguko wa pili tunakwenda kufanya makubwa katika mechi zetu, kuanzia mchezo dhidi ya Azam FC,” Mwagala ametamba.

Mara ya mwisho kwa timu hiyo kupata ushindi ilikuwa ni Desemba Mosi, mwaka jana iliposhinda nyumbani, mabao 2-1 dhidi ya Mtibwa Sugar, lakini baada ya hapo imecheza mechi tano mfululizo.

Tabora United iko kambini kujiandaa kuivaa Azam FC, mechi itakayopigwa Jumatatu kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi huku wakiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao 4-0 katika mchezo wao wa kwanza wa msimu huu 2023/24.

Chanzo: Dar24