Bao pekee la wenyeji lilifungwa dakika ya tatu na nyota wa kikosi hicho, Andy Bikoko na kuhitimisha ukame wa kucheza michezo minane bila ya ushindi tangu mara ya mwisho ilipoifunga Mtibwa Sugar mabao 2-1, Desemba, Mosi mwaka jana.
Baada ya mwenendo mbaya wa matokeo katika Ligi Kuu Bara kwa Tabora United, kikosi hicho kimeonja ladha ya ushindi wa bao 1-0, jana dhidi ya Coastal Union kwenye mchezo mkali na wa kusisimua uliopigwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora.
Bao pekee la wenyeji lilifungwa dakika ya tatu na nyota wa kikosi hicho, Andy Bikoko na kuhitimisha ukame wa kucheza michezo minane bila ya ushindi tangu mara ya mwisho ilipoifunga Mtibwa Sugar mabao 2-1, Desemba, Mosi mwaka jana.
Mchezo huo ni wa 19 kwa Tabora msimu huu ambapo imeshinda minne, sare tisa na kupoteza sita ikiwa nafasi ya tisa na pointi 21.
Kwa upande wa Coastal Union hicho ni kichapo cha kwanza baada ya kucheza michezo sita mfululizo ya Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza tangu mara ya mwisho ilipofungwa mabao 2-1, na Singida Fountain Gate kwenye Uwanja wa Liti Singida Novemba 27, mwaka jana.
katika michezo sita iliyocheza Coastal bila ya kupoteza, ilishinda mitano huku mmoja tu ukimalizika kwa suluhu dhidi KMC Februari 12, mwaka huu na kuifanya kuendelea kushikilia nafasi ya nne kwenye msimamo na pointi 26 baada ya michezo 18.
Baada ya matokeo hayo, Tabora itasafiri kupambana na Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma huku kwa upande wa Coastal United ikiifuata Azam FC kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam, mechi zote zikipigwa Machi 6.