Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tabora United, Thabit Kandoro amesema klabu hiyo imeanza kutekeleza mapendekezo iliyopewa na Bodi ya Ligi (TPLB) ya kuukarabati Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi uliopo Tabora kabla ya hatua hazijachukuliwa.
Akizungumza nasi, Kandoro alisema kabla ya wao kupokea barua hiyo tayari walianza mchakato huo mara moja ili kuuweka uwanja huo katika kiwango bora kitakachokidhi matakwa ya ligi namba tano kwa ubora Afrika.
“Kabla ya kupokea barua yao sisi wenyewe tulijifanyia tathimini ya kina na kugundua kuna maeneo tunapaswa kuyaboresha na tulianza huo mchakato kwa haraka kwa sababu hatutaki kuchezea nje ya mkoa wetu,” alisema.
Kandoro aliongeza jambo nzuri kwao mchezo unaofuata watakaokuwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi utachezwa Oktoba 22 dhidi ya Dodoma Jiji hivyo wana muda mrefu wa kurekebisha kasoro mbalimbali walizoelekezwa kuzifanyia kazi. Timu hiyo ilipanda Ligi Kuu Bara msimu huu.