Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Tabora United yaanza kulipa madeni

Tabora United Mmm Tabora United yaanza kulipa madeni

Sun, 21 Jul 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Mwenyekiti wa timu ya Tabora United inayoshiriki Ligi Kuu Bara, Richard Abwao ambaye pia ni Kamanda wa Polisi mkoani hapa amesema tayari wameanza kulipa madeni waliyokuwa wanadaiwa na wachezaji wao wa nje ili wafunguliwe kuendelea na usajili kwa ajili ya msimu ujao.

Akizungumza na Mwanaspoti leo Julai 20, Abwao amesema wamekuwa kimya kwa muda mrefu wakishughulikia changamoto ya kufungiwa kufanya usajili.

“Kama mnavyojua FIFA walitufungia usajili kwa sababu tulikuwa tukidaiwa na wachezaji hususan Makuntima Kisombe Guylain lakini habari njema ni kwamba tumeshaanza kulipa madeni ili turuhisiwe kusajili tujiandae na msimu ujao ndiyo maana mashabiki wetu hawapati taarifa muhimu kutokana na madeni kuchukua muda mrefu kuanza kuyalipa kwa wahusika.

“Malengo yetu kwa ligi ya msimu ujao ni kuhakikisha tunakuwa na timu ya ushindani ambayo itacheza ligi bila kucheza play off ya kujinasua kushuka daraja, na hatutaki kurejea yaliyotokea msimu uliopita, uongozi wa timu kwa kushirikiana na wadau wengine tumejipanga kuhakikisha Tabora United inarejea ikiwa imara,” alisema.

Hata hivyo mashabiki wa timu hiyo mkoani hapa wamewaomba viongozi wa Tabora United kufanyia kazi changamoto zote zilizosababisha timu yao icheze Play Off ambapo Efraim Naftal amezungumza kwa niaba yao.

“Ukiangalia msimu uliopita timu yetu ilishika nafasi ya pili kwa kuingiza mapato mengi ukiachilia mbali timu za Simba na Yanga, maana yake ni kwamba timu yetu ina wadau wengi ambao wanaweza kuisapoti na ikayafikia malengo, tuwaombe viongozi wawalipe wachezaji ili wawe na morali kwa muda wote wa ligi.

“Kwa mantiki hiyo tunawaomba viongozi changamoto zilizotokea msimu uliomalizika zifanyiwe kazi kwani timu yetu iliingiza shilingi 223,270,000 kutokana na mashabiki kuingia uwanjani, ni fedha nyingi na hatutegemei kuona timu ikipata changamoto kama mwaka jana,” alisema.

Mei 8 mwaka huu Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA) kupitia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lilitangaza kuifungia Tabora United kusajili baada ya kudaiwa na mchezaji Makuntima Kisombe Guylain malimbikizo ya mshahara, wakati huohuo Novemba 7, 2023 walifungiwa kusajili baada ya mchezaji Evariste Kayembe kulalamikia malimbikizo ya fedha za usajili pamoja na mshahara.

Chanzo: Mwanaspoti