Mchezo wa Taifa Stars dhidi ya Uganda ulipigwa jana usiku ulisimama kwa muda kufuatia taa za uwanjani kupungua mwanga wakati mchezo ukiendelea.
Dakika ya 37 mwamuzi wa mchezo Ibrahim Traore alisimamisha mchezo huo kufuatia hitilafu hiyo huku akiwapa nafasi wachezaji kupata mapumziko mafupi ya kupata maji.
Hata hivyo baada ya wachezaji kumaliza dakika Moja ya kupata maji bado taa hizo zilikuwa hazijarudi katika ufanisi wake zikiwaka chache tofauti na wakati mchezo ulipoanza.
Hali hiyo ilileta sintofahamu kwa mashabiki wanaofuatilia mchezo huo huku maafisa wa mchezo huo wakiwemo waamuzi na mechi kamishna wakijadiliana kusubiri muafaka wa kurejea kwa mwanga zaidi.
Tukio hilo lilichukua zaidi ya dakika 15 mpaka mchezo kurejea na mwisho wa mtanange huo wenyeji Stars walikubali kichapo cha bao 1-0.