Benchi la Ufundi la Geita Gold FC limesema kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Tanzania Prisons kumewaumiza sana akili na kwamba wanajipanga upya kumalizia hasira zao kwa Mbeya City wakiahidi hawatarudia makosa.
Geita Gold kwa mara ya kwanza ilipoteza mchezo dhidi ya Prisons lakini ikiharibiwa rekodi yake ya kutopoteza mechi 39 mfululizo kwenye Uwanja wa Nyankumbu mechi 15 za Championship na 24 za Ligi Kuu Bara.
Prisons ndio ilikuwa timu ya kwanza kupata ushindi uwanjani hapo ilipoisulubu Geita mabao 3-1 na kufuta uteja dhidi ya wapinzani hao ambao walikuwa wakiipa upinzani katika mechi walizowahi kukutana.
Hadi sasa Geita Gold ipo nafasi ya tano kwa pointi 37 na imebakiza mechi mbili ikianza na Mbeya City Mei 13, nyumbani kisha kumalizia msimu ugenini dhidi ya Ihefu na Mtibwa Sugar.
Kocha msaidizi wa Geita Gold FC, Mathias Wandiba amesema hawaamini kilichowatokea dhidi ya Prisons na kwamba makosa yaliyojitokeza hawatarajii yajirudie kwenye mechi zilizobaki na kwamba hasira zote ni kwa Mbeya City.
“Kwa ujumla matokeo hayo yalituumiza sana, ila haijirudii, kwa sasa tunajipanga upya kwa mchezo ujao dhidi ya Mbeya City tukihitaji ushindi ili kuendelea kulinda nafasi yetu,” amesema Wandiba.
Amesema wanaamini kwa maandalizi waliyonayo hawapoteza mchezo wowote ili kufikia malengo akiwaomba mashabiki kuendelea kuisapoti timu hiyo hadi mwisho.