Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TPLB yazikumbusha klabu kutii kanuni

Bodi Ya Ligi.png TPLB yazikumbusha klabu kutii kanuni

Thu, 6 Jul 2023 Chanzo: Dar24

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB), imezitaka klabu zote za Ligi Kuu Tanzania Bara, Ligi ya Championship na Daraja la Pili ‘First League’ kuwafanyia vipimo vya afya wachezaji wote watakaowatumia kwa msimu wa mashindano wa 2023/24 ili kutelekeza matakwa ya kikanuni na masharti ya leseni za klabu.

Taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari na Mawasiliano ya Bodi hiyo, imesisitiza kuwa wachezaji wote watakaotumika kwa michezo ya ligi msimu ujao wanapaswa kuwa wamepimwa na kuthibitishwa na daktari kuwa hawana matatizo yoyote yanayoweza, kuhatarisha usalama wao na wachezaji wengine.

“Wachezaji ambao hawatofanyiwa vipimo vya afya na kupata cheti cha utimamu wa afya, watakosa sifa za kusajiliwa na kupatiwa leseni maalum za usajili wa wachezaji zinazotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), hivyo hawatoruhusiwa kucheza mashindano yoyote yaliyo chini ya shirikisho hilo,” imeeleza taarifa hiyo.

Imesema zoezi hilo ni muhimu na la lazima kwa mujibu wa Kanuni ya 69:2 (2.4) ya Ligi Kuu, na ya 70:2.(2.4) kwa Kanuni ya Ligi ya Championship na First League kuhusu maombi ya usajili, hivyo klabu zote zinapaswa kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kikamilifu chini ya daktari mwenye sifa na vigezo vinavyohitajika, huku ikizitakia klabu zote maandalizi mema ya msimu wa 2023/24.

Tayari Klabu ya Simba SC ilianza kuwapima wachezaji wake tangu Jumatatu (Julai 03) kwenye Hospitali ya Rufaa Muhimbili, huku Azam FC yenyewe ikianza zoezi hilo kwenye Hospitali ya Aga Khan, zote za jijini Dar es Salaam.

Chanzo: Dar24