Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), imetangaza uchaguzi mdogo wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), utakaofanyika Dar es Salaam, Disemba 9 mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa na kamati hiyo leo, imeeleza kuwa katika uchaguzi huo, nafasi mbili zitawaniwa ambazo ni nafasi moja ya mjumbe mwakilishi wa klabu za Ligi Kuu ya NBC na nafasi moja ya mjumbe mwakilishi wa klabu za ligi ya NBC Championship.
"Mgombea ni lazima awe Rais/Mwenyekiti wa klabu. Fomu zitaanza kutolewa kuanzia Ijumaa tarehe 13 hadi 17/10/2023 na zitapatikana ofisi za TFF na kwenye tovuti ya TFF na TPLB," ilifafanua taarifa ya mwenyekiti wa kamati hiyo, Wakili Kiomoni Kibamba.
Nafasi hizo mbili zimebaki wazi kutokana na wajumbe wake kupoteza sifa ya kikatiba kuzitumikia.
Nafasi ya mjumbe mwakilishi wa klabu ya Ligi Kuu inajazwa kufuatia kushuka daraja kwa Mbeya Kwanza ambayo mwenyekiti wake, Shiraz Batchu alikuwa miongoni mwa wajumbe watatu wanaowakilisha timu za Ligi Kuu.
Uchaguzi wa nafasi moja ya ujumbe uwakilishi wa Ligi ya Championship unafanyika kutokana na mjumbe aliyekuwa akiishikilia, Japhet Makau hivi sasa kuwa Rais wa Singida Big Stars inayoshiriki Ligi Kuu.