Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TPLB huru ndio dawa gharama za mchezo

Inonga Simba Yanga TPLB huru ndio dawa gharama za mchezo

Tue, 25 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Wakati Azimio la Bagamoyo linafikiwa katika kikao kazi kilichofanyika Bagamoyo mwaka 2007, wadau walikuwa wanataka soka sasa liendeshwe kiweledi zaidi kwa kila mmoja kuwajibika na majukumu yake badala ya mmoja kubeba majukumu yote.

Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) liliitisha kikao hicho kati ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na wadau wake, hasa klabu ambao ndio washiriki wakubwa wa soka la kila siku, kwa maana ya mashindano.

Mada zilihusu ufanisi katika uendeshaji soka na nini kifanyike ili kubadili muundo na kuwezesha kila upande ujishughulishe na majukumu yake na kuwa na ufahamu mpana na hatimaye kubuni mbinu za kuendeleza eneo lake.

Kwa nchi kama England, maendeleo yamefikia kiwango kwamba hata waamuzi wana chombo chao ambacho ni kampuni, kinachojishughulisha na maendeleo ya taaluma hiyo, maslahi na mafunzo.

Hiyo ina maana kwamba Chama cha Soka cha England (FA) kinajishughulisha zaidi na programu za maendeleo, sera, kanuni na kesi zinazohusu matatizo yanayotokea katika uendeshaji ligi, na mambo mengine ya shughuli za kila siku.

Ndio maana kocha akifanya makosa, hushtakiwa FA na si FA kumshtaki kocha huyo halafu kamati yake ndio ije imuhukumu. Hapana, chombo kinachoshtaki ni kingine ambacho kinaweza hata kubaini kasoro kwa mshtaki, ingawa wenzetu ni makini mno na hawana zengwe.

Na huko ndiko kulikoanzia ligi kujiondoa kwenye mikono ya vyama vya soka vya nchi.

Mwishoni mwa msimu wa soka wa 1990/91, kuliwasilishwa pendekezo la kuanzishwa kwa Ligi Kuu ya England ambayo ingekuwa huru kujiendesha na isiyo chini ya FA. Klabu zote 18 zilizokuwa zinashiriki Ligi Daraja la Kwanza zilikubaliana na pendekezo hilo na baadaye FA ikaonyesha kukubaliana nalo katika chapisho lake la mwongozo wa kuendeleza soka.

Klabu hizo zikasaini makubaliano ya wanachama waasisi mwezi Julai mwaka 1991 na huo kuwa mwanzo wa Ligi Kuu ya England (EPL), kuwa chombo huru kinachojiendesha bila ya kuingiliwa na hata robo ya mkono wa FA.

Maana yake, EPL iko huru kubuni kanuni zake ambazo zinaona zitanufaisha klabu na kuifanya ligi hiyo kuwa bora zaidi duniani na kuvutia wadau wote; wakiwemo wawekezaji, wadhamini na wanasoka wa kimataifa.

Hapo huwezi kujifungia na kutunga kanuni zako bila ya wawakilishi wa klabu, ukasaini mikataba ya udhamini ya Ligi Kuu wakati wenye ligi wapo, ukasaini mikataba ya haki za matangazo wakati wenye mpira wapo.

Hayo yote yanamaanisha maslahi kwa klabu. Yaani kanuni zinazosimamia uendeshaji wa ligi na masuala ya mgawanyo wa mapato zinatungwa na wenye ligi wenyewe kwa kuzingatia mazingira ya wakati huo, kama upatikanaji wa viwanja na gharama zake ili kunufaisha pande zote.

Hata mikataba ya udhamini au haki za matangazo ya televisheni hujadiliwa kwa kina na wenye ligi, yaani klabu na si kuletewa donge ambalo kwa nje huonekana kubwa kumbe ndani halisaidii sana wahusika.

Wahusika na gharama za mechi ni lazima watajwe kwenye kanuni ambazo zimejadiliwa kwa mapana na marefu na wahusika badala ya kikundi cha watu wasiowajibika kwa klabu bali wanaowajibika kwa chombo kingine kisicho na machungu na ligi.

Pale ambapo kutaonekana matatizo, klabu hushikana mashati kuhakikisha haki inatendeka kwa kuwa sababu moja isipotendewa haki kwa kuni fulani, kesho mpira utaigeukia timu fulani, kwa hiyo umakini mkubwa unauwepo kuhakikisha haki inatendeka kwa wote.

Kwa muundo wa sasa wa uendeshaji soka nchini, yale malalamiko kwamba waamuzi wanachezesha kwa maelekezo, hayawezi kuisha kwa kuwa marefa wanawajibika kwa TFF na si wenye mpira ambao ni klabu. Unapokuwa na chombo imara cha klabu kinachosimamia ligi, lawama hizo zitahamia kwa waamuzi kwamba ama wamechukua fedha ama hawajui sheria badala ya lawama za “kuchezesha kwa maelekezo.

Nimeanzia mfano huo mkubwa kutaka kuweka picha katika suala zima la mgawanyo wa mapato na hasa suala la gharama za mechi ambalo kadri siku zinavyokwenda ndio linazidi kugeuza viongozi wa TFF, Bodi ya Ligi Kuu (TPLB) na wa klabu kuwa mabubu kwa kuwa wanazidi kuwa sehemu ya tatizo.

Wadau wanaona kuna tatizo, lakini viongozi wa pande zote wamegeuka mabubu. Hawajitokezi hata kufafanua kuwa tatizo kama hilo halipo licha ya kipengele hicho kusomba mamilioni ya fedha kama nilivyoeleza katika makala yangu ya jana. Kwa kuwa viongozi wa klabu wanaona yuko wa kurushiwa lawama, wanakuwa sehemu ya tatizo na kwa kuwa pande nyingine zinaona wahusika wanashiriki, nao hawaoni sababu ya kulivalia njuga.

Lakini kama TPLB ingekuwa ni chombo halisi cha klabu na kinawajibika kwa klabu badala ya TFF, ni lazima kasoro zisizokuwa na msingi zingepungua. TPLB ndio ingekuwa inaibuka na mapendekezo lukuki kila mwishoni mwa msimu, kuyasambaza kwa klabu na baadaye kuyajadili katika vikao kazi kabla ya kupitishwa na mkutano mkuu.

TPLB ingekuwa na meno hayo na inawajibika kwa klabu badala ya TFF, klabu zingekuwa na nguvu ya kuikabili na kupambana nayo katika masuala ya usimamizi wa ligi, kumiliki michezo yake na masuala mengine.

Ilikuwa ni ajabu kwamba mtendaji mkuu wa Simba wakati huo, Barbara Gonzalez alizuiwa kuingia uwanjani na watendaji wa TPLB katika mechi ya ligi ambayo Simba alikuwa mwenyeji. Ni kituko!

Kule Afrika Kusini, ambako Ligi Kuu inaweza kuzuia wachezaji wa klabu kwenda kuchezea timu ya taifa katika tarehe ambazo si za Fifa, Kaizer Chiefs ilizuia mchezo wake wa ligi kuchezwa kutokana na tatizo la ugonjwa wa virusi vya corona, Covid-19.

Ligi Kuu ilikataa kuahirisha mechi licha ya wachezaji kadhaa wa Kaizer kugundulika kuwa na maambukizi. Siku hiyo, waamuzi walienda uwanjani kama kawaida, lakini getini wakakuta milango imefungwa na wana usalama hawaruhusu mtu yeyote kuingia na mechi haikufanyika. Hakuna hatua zilizochukuliwa dhidi ya vigogo hao.

Ni kweli kwamba uhuru huo umezidi viwango, lakini hiyo inaonyesha ni kwa kiasi gani klabu zina nguvu katika kuhakikisha utaratibu unazingatiwa na si kusubiri FA ikosee kama walivyofanya Yanga siku ya mechi na Simba.

Kwa hiyo dawa pekee ambayo inaweza kupunguza tuhuma dhidi ya utafunaji wa mgawo wa mapato, na hasa gharama za mechi, ni klabu zenyewe kuishika ligi na kuhakikisha zinashiriki kwa kiasi kikubwa kutengeneza kanuni ambazo zitazinufaisha klabu.

Ile kauli kwamba tulipeleka kanuni kwa klabu lakini hakuna aliyejibu, zitaisha kwa kuwa klabu zitakuwa zinajua kuwa TPLB ni chombo chao na kisiposikiliza ushauri wao, viongozi wataondolewa na kuwekwa ambao watawajibika kwa klabu na si shirikisho.

Sehemu yoyote duniani, maendeleo yalikuja baada ya kuwepo kwa mgawanyo wa majukumu. Ifike wakati kila chomo kihusike na eneo lake. Chama kihusike katika maendeleo na utoaji sera na dira, Ligi Kuu iendeshwe na klabu zenyewe na hata waamuzi wawe na chombo chao huru. Kila mmoja ahesabu yake, tuone nani atapiga hatua.

Chanzo: Mwanaspoti