Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TPLB, TFF wapata mwarobaini wa waamuzi

VAR Bongo.jpeg TPLB, TFF wapata mwarobaini wa waamuzi

Sun, 4 Dec 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Bodi ya ligi kuu nchini (TPLB) imesema ili kuondokana na changamoto za waamuzi inakusudia kuleta vyombo vya kiteknolojia kama ilivyo ligi za mataifa mengine ikiwamo kombe la dunia.

Pia imesema hadi sasa inaridhishwa na mwenendo wa ligi ya championship kutokana na kupungua kwa malalamiko lakini zikionesha ushindani hivyo wanatarajia timu zilizojiandaa zitaweza kupanda daraja.

Miongoni mwa mataifa yanayotumia vifaa vya kiteknolojia (V.A.R) kwenye ligi kuu kuwasaidia waamuzi katika majukumu yao uwanjani ni pamoja na England na sasa Tanzania inakusudia kuleta vyombo hivyo ili kumaliza changamoto na malalamiko juu ya marefa.

Akizungumza Mtendaji Mkuu wa bodi hiyo, Almas Kasongo amesema Mamlaka za soka na serikali tayari wameshaliona suala la waamuzi na zipo juhudi za makusudi wanatarajia kuzifanya ili kuondokana na kutegemea na kuamini 'makosa ya kibinadamu' kwa waamuzi kuhakikisha siku za usoni wanaleta vifaa vya kiteknolojia kama ilivyo mataifa mengine.

Amesema kwa sasa wanaendelea kufuatilia kwa ukaribu ligi zote kuhakikisha zinachezwa kwa haki na mshindi anapatikana kihalali ndani ya dakika 90 na ndio maana wanafika viwanja tofauti kushuhudia mechi.

"Dunia ya sasa imeshatoka huko, bodi ya ligi, TFF na serikali tumeliona na tunafanya juhudi za makusudi kuhakikisha tunaleta vyombo vya kiteknolojia kuwasaidia waamuzi na kuondokana na malalamiko, kwa ujumla tunaridhishwa na mwenendo wa championship " amesema Kasongo.

Kuhusu udhamini, kigogo huyo amesema hadi sasa wapo kwenye mazungumzo ya mwisho na watu kama watatu ambao muda wowote wakikamilisha wataweka wazi.

Amesema TPLB kwa kushirikiana na shirikisho la soka nchini (TFF) wamekamilisha mazungumzo na shirikisho la soka duniani (FIFA) kupitia mradi wa 'Fifa plus' kutangaza 'live' ligi ya Championship na First League ambapo mapato yatakayopatikana yatarudi kwa timu zenyewe.

"Hii itazisaidia timu za Championship, First League na Ligi ya Wanawake, niwaombe wadau, mashabiki 'ku-subscribe' ili kuongeza kipato kwa timu zetu, sisi mamlaka tunaendelea na juhudi kuhakikisha tunapata wadhamini" amesema Kasongo.

Chanzo: Mwanaspoti