Wakati mshambuliaji wa Wydad Athletic Simon Msuva akidaiwa kuwindwa na TP Mazembe ya DR Congo klabu hiyo imefunguka juu ya mchezaji huyo.
Mkurugenzi wa Utawala wa Mazembe Andrea Mutini amesema wanaheshimu ubora wa Msuva lakini hayupo katika hesabu zao kwasasa.
Mutini ambaye siku chache zilizopita alikuwa nchini kuja kuchukua kiungo wa Yanga Mukoko Tonombe amesema Mazembe haijamuhitaji mshambuliaji hhuyo.
"Tumeona tu hizo taarifa katika mitandao mbalimbali na tuseme Msuva ni mchezaji mzuri na bora," amesema Mutini.
"Sijaona pendekezo la kocha au hata sisi kama viongozi kumtaka Msuva nakumbuka hata nilipokuwa hapo Tanzania kiongozi mmoja aliniuliza kuhusu hilo.
Bosi huyo ameongeza katika dirisha la usajili linalofungwa leo usiku nchini DR Congo wataingiza wachezaji wawili pekee.
" Hapa kwetu dirisha la usajili linafungwa leo usiku na nakuthibitishia tutasajili watu wawili pekee dirisha hili dogo ambao ni Mukoko na mwingine mmoja lakini sio Msuva."
Msuva bado yuko nchini akionekana kujifua kwa mazoezi makali huku ikielezwa yuko katika mgogoro na uongozi wa klabu yake ya Wydad ingawa mwenyewe amekuwa hataki kuliweka wazi suala hilo.