Wakati kukiwa na kila dalili za hofu kwa Mashabiki juu ya ujio wa klabu bora ya Soka kutoka Congo, TP Mazembe, Uongozi wa Klabu hiyo umewatoa shaka mashabiki na kudai utawasili mapema tu kuja kukipiga na Simba SC katika kilele cha Tamasha la Simba Day.
Kaimu Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga amesema kuwa mashabiki wasiwe na hofu TP Mazembe itawasili Dar na mchezo utachezwa bila mashaka.
“Kumekuwa na hofu juu ya ujio wa TP Mazembe lakini ninapenda kuwahakikishia mashabiki wa Simba kwamba timu hiyo inakuja na tunatarajia kuwapokea Septemba 18 kisha mchezo utakuwa Septemba 19.
“Hakuna sababu ya kuwa na mashaka juu ya hilo kwani wenyewe wamethibitisha hiyo tunaamini kwamba watakuja. Utaratibu mzuri wa kuwapokea utapangwa na mashabiki wataiona timu itakavyotua.
“Maandalizi kiujumla yanakwenda sawa kwani kuanzia zoezi la uuzaji wa tiketi kwa ajili ya Simba Day pamoja na namna ambavyo mashabiki walivyopanga kuwasili Uwanja wa Mkapa kwa wale ambao wanatoka nje ya Dar ulivyo ni mzuri na wameamua kuweka makutano kuwa Morogoro hivyo kuna mengi yanakuja,” amesema Kamwaga.
Mechi ya Simba na TP Mazembe Septemba 19 kwa Mkapa Dar es Salaam, ndio itakuwa mechi ya kwanza ya wazi kwa Mashabiki wa Simba ambao wana hamu kubwa ya kuona kiwango cha timu yao hasa usajili wa wachezaji wapya ambao walipambwa kupita kiasi na viongozi wa Simba.