Mpira ni sayansi. Hiyo ni kauli ya Mkurugenzi wa Ufundi wa Azam FC, Dk Jonas Tiboroha anayeamini ndiyo dira ya mafanikio katika mchezo huo.
Katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Dk Tiboroha amezungumzia mambo mengi yanayohusu soka la Tanzania huku akiweka wazi mipango na malengo ya Azam FC.
AZAM TISHIO
Dk Tiboroha anakiri kuwa licha ya Azam FC kuwa na uwekezaji mkubwa itakuja kuwa klabu tishio Afrika Mashariki baada ya Tanzania kupata matunda kutokana na uwepo wao.
“Sio kwamba Azam haijafanya chochote, naona watu wanauliza Azam inafeli wapi. Nadhani sio kweli na napingana nao kwa sababu klabu nyingi hapa nchini zina wachezaji kutoka Azam kwenye ligi mbalimbali.
“Kwangu kitendo cha wachezaji wao wengi kushiriki ligi hizo, kwa upande wa nyumbani Azam ina mchango wake mkubwa. Labda kimataifa, na ndio maana tumekuja kufanya kitu,” anasema.
Anasema kwa sasa malengo makubwa ni kuhakikisha Azam kupitia akademi yao inazalisha nyota wengi ambao watakuwa na faida ndani na pia nje kwenye timu nyingine.
AWAKATAA MAPRO
Kwa sasa klabu zinaruhusiwa kusajili wachezaji wa kigeni 12 ambapo hupata nafasi ndani ya timu wakiwa wanane, kitendo kilichopigwa vikali na wadau mbalimbali wa soka wakiamini jambo hilo linaua timu ya taifa.
Dk Tiboroha anasema: “Mapro 12 daah! Tulianza na saba tukaja 10, tumeongeza tena kwa manufaa gani. Sasa tunakoelekea tutaku-wa nao hadi 20. Ta-yari hizi programu zetu za vijana ambazo tunazifanya zitakuwa zinapotea na hazina afya,” anasema.
Dk Tiboroha aliyewahi pia katibu mkuu wa Yanga, anasema idadi hiyo inazidi kulipeleka soka shimoni na hakuna hamasa hususan katika timu ya taifa.
“Wachezaji ambao tunatakiwa kuwatumia katika timu za taifa ni wale ambao unakuta timu zao za ndani hawachezi kabisa, lakini ningekuwa mimi tungetakiwa kufanya programu nyingi za vijana - kama sisi Azam tunavyofanya ambazo zingetuzalishia wachezaji wenye uwezo mkubwa,” anasema na kuongeza kuwa ingekuwa hiari yake walau mapro wangesingezidi watano kutokana na mfumo ulivyo.
MALENGO AZAM
Kiongozi huyo anasema lengo kubwa la Azam ni kuzalisha wachezaji ambao wataendelea kuitangaza Tanzania, lakini kupitia Azam FC na ndio maana wanakomaa kuanzia chini kwa vijana ambao ndio chimbuko la ufaulu.
“Ili uweze kufikia malengo hakuna ubishi ni lazima uanze na vijana huku chini, maana tuna timu nyingi za watoto ambao hao wakiendeshwa katika misingi na mfumo wa kisoka itawafanya wazidi kuwa bora zaidi.”
Anasema alitua Azam kama mshauri na anaamini kwa uwezo alionao kila kitu kitaenda vyema kwa ushirikiano na wenzake.
“Ukiangalia Saimon Msuva, Himid Mao wote wametoka Azam kina Manula (Aishi) na wanafanya vizuri huko waliko na ni zao la Azam, sasa tunapambana kuwazalisha wengine,” anasema na kuongeza kuwa wanatazama soka la wachezaji hivi sasa linahitaji nini.
MCHUJO WACHEZAJI
Dk Tiboroha anasema kuna mifumo mingi ambayo wameitengeneza kwa vijana na ikitokea mchezaji hajiwezi wanamuacha na kuchukua ambaye anajiweza.
Anakiri kuwa ili kupata mchezaji bora ambaye atakuwa na manufaa makubwa baadaye wanaangalia mpaka vimo vya wachezaji husika. Wanatizama wanahitaji mshambuliaji wa namna gani na mlinda mlango wa namna gani ndicho kitu ambacho wanakihitaji.
Hata kuhusu makocha ambao wanazinoa timu hizo sio tu kuibuka na kwenda kuwafundisha, bali wanatazama mambo mengi na kuhakikisha kunakuwa na nguvu kazi kubwa ambayo italeta mabadiliko.
“Ukiona kitu chenye mafanikio kinakuja haraka ujue hakuna ishu hapo. Kitu kizuri kinakuja taratibu na kufikia malengo ndio maana ya mabadiliko hayo,” anasema.
NENO KWA VIONGOZI
Mtalaamu huyo wa soka anasema Tanzania inakwenda kwa mfumo kwa kuwa watu wanaamini michezo ni mtu yeyote anaweza kuendesha bila ya kufahamu kuwa ni sayansi.
“Watu wanaamini michezo ndio uwachukue wacheza mpira wa zamani.. sijui nini, lakini wanashindwa kufahamu mpira wa kisasa unahitaji kufahamu unahitaji nini kifanyike ili uweze kufanyika.
“Waswahili wengi wanaona tu mpira wanajua ni kujiendea tu. Kuna watu wanajiita mameneja mara maajenti wanajua tu ni kumchukua mchezaji kumtoa pointi A kwenda B, bila ya kujua wala kufahamu hiyo pointi B inahitaji mchezaji husika awe na nini.
“Ukimuuliza meneja naomba wasifu wa mchezaji wako kwa nini nimchukue utasikia blahblah tu, ila vitu vya msingi kwa mtu mwenye weledi wa mpira huwezi kuvipata,” anasema na kuongeza kuwa wanaosema ovyo ndio wanasikilizwa kuliko wenye sayansi ya mpira.
AFUNGUKiA Leseni ya klabu
Anasema wakati akiwa Shirikisho la Soka nchini (TFF)alibaini kuwepo kwa changamoto ya ukosefu wa ushirikiano wa kutosha baina ya TFF na klabu husika.
“Nilipokuwa pale toka 2014, suala la club licence (leseni ya klabu) hasa kipengele cha vijana, hatuoni klabu zikifuata mifumo hiyo,” anasema.
“Tunaona klabu zinakuwa na timu za vijana kukiwepo na mashindano fulani, lakini shirikisho hawafuatilii. Sisi Azam kwa sasa tuna timu ya U-9, U-15, U-17 pamoja na U-20 na timu ya wakubwa.”
Anasema kama TFF wasipotilia mkazo suala la leseni, taifa halitafika kokote kwa kuwa mpira mzuri unaanzia kwa vijana huku akiwataka kufuata misingi ya utawala bora ambao ndio utawafanya wao kufanya kazi na kila mmoja.
“Lakini ukianza kusema hili ni koleo na hiki ni kijiko, hili kubwa hili dogo na vyote vinafanana itakuwa haipotezi maana. TFF wanatakiwa kutoangalia sura ya mtu na nani anayekuja kusema nini na sheria zifuate, hiyo ndiyo misingi ya utawala bora kwa sababu uwezo tunao,” anasema.
ISHU YA UMRI YAMKERA
Katika kuhakikisha soka linakua, Dk Tiboroha anawataka wadau wa soka kuacha udanganyifu katika timu za vijana ilimradi kufanikisha mambo kwa wakati bila ya kujua madhara yake ni yapi.
“Unakuta timu unaambiwa U-17 na U-20, lakini ukiwaangalia unawaona kabisa hawa ni U-40 sasa tunajidanganya wenyewe jambo ambalo si zuri kwa afya ya soka hata kidogo. Unakuta mchezaji ana miaka 25 au 26 halafu unaambiwa yuko U-20 unajiuliza hawa watu shida yao nini hata majibu haupati,” anasema.
Anasema udanganyifu huo sio mzuri na ni kujidanganya wenyewe, lakini akisisitiza pia ni jambo linalotokana na mfumo kutokuwa mzuri badala ya kujua soka ni taaluma na biashara.
UDHAMINI, UWEKEZAJI
Dk Tiboroha anasema Ligi Kuu ni ngumu msimu huu na inachagizwa na namna ambavyo wadhamini wamejitosa kuwekeza.
“Mfano Azam ameweka pesa nyingi sana na kila timu inakuwa na uwezo na uhakika wa kufanya usajili mzuri kuanzia wachezaji na hata makocha. Kila timu inajua inacheza na inapambania kitu kikubwa. Hata ushindani unaonekana ulivyo,” anasema.
Kuhusu uwekezaji wa klabu, anasema soka la sasa haliepukiki kuwekeza kutokana na mpira kuhitaji pesa na haiwezekani timu ilalamikie maisha magumu kama ilivyokuwa nyuma.
UBINGWA MSIMU HUU
Kwa namna ambavyo Azam FC ilivyo msimu huu, Dk Tiboroha anasema anaamini lolote linaweza kutokea katika kusaka taji la ubingwa Ligi Kuu linaloshikiliwa na Simba msimu wa nne mfululizo. “Timu yetu ya Azam inafanya vizuri. Ukiangalia hata katika michezo saba ambayo tumecheza hatujafanya vibaya hata kidogo. Nakumbuka hata Manchestar City waliwahi kuanza hivi kama sisi, lakini walikuja kulitwaa taji hilo. Unajua ni bora kuanza hivi kuliko kumaliza vibaya unashindwa kujipanga,” anasema na kuongeza kuwa ni vizuri kuanza vibaya ukianza vizuri unaridhika na kuona kuwa umemaliza kazi.
Anasema katika kikosi wanao wachezaji wapya, hivyo itawachukua muda kidogo kuzoeana na wenzao, lakini sio sababu ya wao kutofanya vizuri.
AFUNGUKiA USAJILI
Timu za Tanzania hususan Simba, Yanga na Azam zina kasumba ya kugombea wachezaji katika usajili jambo ambalo Dk Tiboroha analiunga mkono kwa kuwa linalotokea duniani kote.
“Kugombea mchezaji kwenye usajili si jambo geni. Ukiona hivyo mchezaji anakuwa na kitu ndani yake na ndio maana inakuwa hivyo, kama asingekuwa na kitu isingetokea hivyo,” anasema na kuongeza kugombea huko kuwe na misingi bora ya kuongeza ushindani kwa waliopo.
Dk Tiboroha mbali na ubobezi wake katika soka, pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam katika Idara ya Sayansi ya Michezo na anakiri kuwa katika maisha yake anapenda soka la vijana akiamini ndiko mastaa wa baadaye waliko na kabla ya kutua Azam aliwahi kupita Yanga akawa katibu mkuu wa klabu hiyo.