Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

THE MVP - Donisia Minja ana balaa kubwa WPL

IMG 4257.jpeg THE MVP - Donisia Minja ana balaa kubwa WPL

Fri, 9 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

JKT Queens ndio mabingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) msimu huu wakiwa wamechukua ubingwa bila kupoteza mchezo wowote.

Licha ya ubora wa kikosi chao lakini safu ya ulinzi ya timu hiyo ilifanya kazi kubwa sana msimu huu na kumaliza ligi ikiwa ni timu iliyoruhusu mabao machache zaidi (manane) sawa na Simba Queens.

Licha ya kwamba kuna kipa na mabeki wake waliofanya kazi safi ndani ya JKT Queens lakini huwezi kumuacha nyuma kiungo mkabaji na nahodha msaidizi Donisia Minja ambaye alikuwa ni kama roho ya safu ya ulinzi ya kikosi hicho.

Donisia alikuwepo kila mpira ulipokuwepo, akikaba vema, akipokonya mipira lakini kubwa zaidi akifunga mabao makali yaliyokuwa yakiwapa pointi muhimu timu yake.

Kiungo huyo mkabaji pia ameingia katika kuwania tuzop ya mchezo bora wa mwaka inayotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) akipambana na Jentrix Shikangwa wa Simba Queens na Amina Bilal wa Yanga Princess.

SIRI YA KUWA MFUNGAJI MAHIRI

Unaweza kushangaa lakini ndio kweli kwani licha ya Donisia kucheza nafasi ya kiungo mkabaji kwenye kikosi cha JKT Queens lakini amemaliza ligi akishika nafasi ya pili kwa ufungaji bora akiwa amefunga mabao 17 nyuma ya kinara Jentrix Shikangwa wa Simba Queens aliyefunga 19. Achana na ubora wa kuzifumania nyavu tu alionao pia ni fundi wa kufunga kwa kutumia mipira iliyokufa (fri-kiki).

Kati ya mabao 17 aliyofunga msimu huu, mabao saba amefunga kwa frikiki na amekuwa na ubora huo kutokana na kufanya sana mazoezi.

"Nimefunga mabao mengi msimu huu kwa sababu ya kujituma, kusikiliza maelekezo ya kocha na kuwa na utulivu ninapokuwa karibu na goli.

"Nafunga sana mabao ya frikiki kwa sababu nayafanyia sana mazoezi. Tukishamaliza mazoezi ya timu kocha ananipa mazoezi maalumu ya kufunga kwa faulo kila siku hivyo nawekewa mipira zaidi ya 10 kufanya zozezi hilo, "anasema Donisia.

LIGI YA MSIMU HUU HATARI

Donisia anasema tangu aanze kushiriki Ligi Kuu Bara, msimu huu wa ligi umekuwa wa tofauti sana kwani ubora ulikuwa mkubwa kwa timu zote shiriki. "Kila timu ilijiandaa ya ani ulikuwa msimu mgumu sana, ndio maana unaona timu nyingi zimepishana kuanzia pointi moja hadi tatu.

"Pia watu wameona jinsi bingwa alipatikana katika mechi ya mwisho ya kufunga msimu sasa hiyo inakupa picha ulikuwa msimu wa aian gani, yaani tulipambana hasa, "anasema Donisia.

MECHI HIZI HATAZISAHAU

Anasema hakuna mechi iliyowapa presha kubwa katika mbio zao za kuwania ubingwa kama ile dhidi ya Yanga Princess iliyofanyika Mei 3.

"Ile mechi na Yanga ilitupa presha sana kwani kumbuka tulikuwa tunakimbizana zaidi na Simba na tulipishana pointi moja tu sasa kama tungepoteza ile mechi ubingwa ilikuwa basi tena.

"Sasa ile mechi ya Yanga bwana, kabla ya mechi tukakaa kikao tukaambiana jamani hii ndio kama fainali kwetu tupambane, tukabe bila kuchoka hadi tushinde na Mungu akatusaidia tukashinda hiyo mechi.

Pia mechi nyingine ambayo ilikuwa ngumu kwetu msimu uliopita ni dhidi ya Amani ya mzunguko wa kwanza yaani tulihangaika ile mechi kutafuta ushindi na ukizingatia ile siku mvua ilinyesha yaani walitusumbua mno tukaja kupata bao moja mwishoni, "anasema Donisia.

CHANGAMOTO YA LIGI

Donisia anasema licha ya msimu huu wa ligi kuwa bora kutokana na ushindani ambao timu zimeonyesha lakini ukosefu wa wadhamini bado ni changamoto kubwa kwenye soka la wanawake.

"Kama wadhamini wakijitokeza wengi basi Tanzania itakuwa na ligi bora sana ya wanawake kwani kwa sasa timu zinapambana zenyewe na nyingi hazina fedha ndio maana unaona kuna wakati nyingine zinashindwa kufika kwenye vituo vya mechi kwa wakati kwa sababu ya ukosefu wa fedha.

"Ndio maana natamani timu ziongezeke lakini hata kama zitaongezeka bila mdhamini ni kazi bure hivyo kama zikiongezeka basi kuwe na wadhamini wa kutusapoti lakini kama hakuna hawatapatikana basi bora zibaki timu 10 kama zilivyo sasa, "anasema Donisia.

JKT QUEENS ILISTAHILI UBINGWA

JKT Queens ndio mabingwa wa Ligi Kuu Bara ya Wanawake iliyomalizika hivi karibuni hivyo kutwaa ubingwa mara tatu tangu ligi hiyo ianzishwe rasmi mwaka 2017.

Ubora wa kikosi chao msimu huu ndio siri kubwa ya JKT Queens kutwaa ubingwa bila kupoteza mechi yoyote kama anavyosema Donisia.

"Kwa kweli tulistahili licha ya kwamba hatukuwa na kikosi bora sana ila tulikuwa na ubora wa wastani na wachezaji tulikuwa na ari ya kujituma sana uwanjani.

"Unajua msimu huu karibu wachezaji wetu wengi walirejea kikosini tofauti na misimu miwili ya nyuma ambayo tulifanya vibaya kwa sababu wachezaji wetu wengi walihamia timu nyingine na pia wengine tulikuwa kozi sasa jambo hilo liliathiri timu yetu.

"Msimu huu wale waliokuwa kozi tulirejea na hata waliokwenda timu nyingine baadhi wamerudi hivyo kurejesha ubora wetu kwa kiasi fulani, "anasema Donisia.

KIKOSI CHAKE BORA MSIMU HUU

1.Najiat Abas (JKT Queens) 2.Anastazia Nyandago(JKT Queens), 3.Fatuma Makusanya (JKT Queens), 4.Happynes Mwaipaja (JKT Queens), 5.Anastazia Katunzi (JKT Queens), 6.Donisia Minja (JKT Queens), 7.Asnath Ubamba(Fountain Gate Princess), 8.Amina Ally (Yanga Princess), 9.Stumai Abdallah (JKT Queesn), 10.Jentrix Shikangwa (Simba Queens) , 11.Pambani Kuzoya (Simba Queens)

Donisia alianza kucheza soka katika shule ya msingi Airwing mwaka 2004 na mwaka uliofuata akajiunga na shule ya sekondari ya Lord Baden Powell ambapo huko aliendelea kucheza huku akishiriki mashindano mbalimbali Umisseta.

"Sasa wakati tunashiriki mashindano mbalimbali shuleni kuna timu ilikuwa inaitwa Uzuri Queens ilikuwa inakuja shuleni kwetu na kutuchukua tukacheze mechi.

"Uzuri Queens wakati huo ilikuwa inashiriki ligi ya wanawake ambao haikuwa rasmi ambayo ilikuwa inashirikisha timu kama nane hivi na niliendelea kuichezea hiyo timu hadi mwaka 2009 niliposajiliwa an Simba Queens ambayo kwa muda mfupi niliocheza hapo nikachaguliwa timu ya Taifa chini ya miaka 20, "anasema Donisia.

Anasema aliichezea Simba hadi mwaka 2014 na kisha kujiunga na Evergreen na baada ya msimu mmoja akasajiliwa na JKT Queens na kufanikiwa kutwaa ubingwa mara mbili mfululizo msimu wa 2017/2018 na 2018/2019 na amekuwa katika kikosi cha maafande hao hadi sasa walipotwaa tena ubingwa msimu huu.

Chanzo: Mwanaspoti