Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TFF yazibeba Simba, Yanga CAF

Simba Yanga Robo CAF TFF TFF yazibeba Simba, Yanga CAF

Tue, 19 Mar 2024 Chanzo: Mwanaspoti

Kabla timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, kuondoka jana kuelekea Azerbaijan, kucheza mashindano mapya na mafupi ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) yajulikanayo kama FIFA Series, kilifanyika kikao kizito kati ya mabosi wa Simba na Yanga kuomba fea.

Simba na Yanga zimeliomba shirikisho hilo kuwaruhusu wachezaji wake kurejea kambini mapema ili waweze kujiandaa vyema na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo Yanga itacheza na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini Machi 30 na Simba dhidi ya Al Ahly ya Misri Machi 29 mechi zote zikipigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Ofisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo jana alisema kuwa wamepokea maombi hayo ya Simba na tayari wameshawajibu kuwa wachezaji wale mastaa wataruhusiwa kurejea nchini baada ya mchezo wa kwanza dhidi ya Bulgaria, Machi 22.

Alisema hawawezi kuruhusiwa wote, lakini anaamini wale wenye umuhimu zaidi kwenye mechi hizo za kimataifa watarudi na wachache watabaki kwa ajili ya mchezo wa pili dhidi ya Mongolia Machi 25.

“Ni kweli kimefanyika kikao na maombi ya Simba na Yanga yalikuwa ni kuomba kama kuna uwezekano wachezaji wao warejee nchini kabla ya mchezo wa pili dhidi ya Mongolia, maombi yao yamepitishwa, lakini siyo wachezaji wote watakaorudi ni baadhi tu, wengine watabaki hadi mchezo wa mwisho.

Mastaa wa timu hizo waliopo katika kikosi cha Stars ni Kibu Denis, Aishi Manula, Mohammed Hussein na Kennedy Juma (wote kutoka Simba), wakati kutoka Yanga wapo Clement Mzize, Aboutwalib Mshery, Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Hamad ‘Bacca.

Stars iliondoka jana alfajiri ikiwa na wachezaji 23 chini ya kocha Hemed Suleiman ‘Morocco kwa ajili ya mechi za kundi la Stars linaloundwa na timu za Bolivia, Mongolia na wenyeji Azerbaijan. Michuano hiyo mipya ya kirafiki ambayo haina zawadi wala kombe, inahusisha timu za kutoka mabara yote. Fifa inagharamia kila kitu. ikiwamo usafiri na malazi kwa timu zote za taifa zinazoshiriki.

Chanzo: Mwanaspoti