Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TFF yamshushia rungu Eymael

2a7324410841ce63d2a56bf7cc39f024 TFF yamshushia rungu Eymael

Tue, 4 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limetoa adhabu ya kumfungia miaka miwili pamoja na faini ya Sh milioni 8, aliyekuwa kocha wa Klabu ya Yanga, Luc Eymael.

Eymael alikuwa akituhumiwa kwa kutoa kauli za kibaguzi kwa Yanga pamoja na kuishambulia TFF alizozitoa baada ya kumalizika kwa mchezo wa kufunga pazia la Ligi Kuu Bara 2019/20 dhidi ya Lipuli FC.

TFF kupitia kwa kamati yake ya nidhamu imemkuta na hatia kocha huyo raia wa Ubelgiji katika kikao cha Agosti 1, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mjumbe wa Kamati ya Nidhamu ya TFF, Alex Mushumbusi, alisema kuwa adhabu hizo zimetolewa baada ya kupitia ushahidi na kujiridhisha kuwa Eymael alitenda kosa.

Alisema kuwa Eymael aliandikiwa barua ya kuitwa katika kikao hicho ili kutoa utetezi wake, lakini hakutokea badala yake alitoa taarifa kuwa wanasheria wake wapo Tunisia.

Aliongeza kuwa kutokana na sheria kuwaruhusu kusikiliza shauri upande mmoja, hivyo haikuzuia kufanyika kikao na kutoa uamuzi huo.

“Tulizisikia kauli zake na tukajiridhisha kuwa ile sauti ni yake, tulipomwita katika kikao cha kutoa uamuzi, yeye alitujibu kwa barua kuwa mawakili wake hawapo nchini wapo Tunisia, tukapima majibu yake tukaona hakuwa na nia ya kuja, tukasikiliza shauri upande mmoja kwa kuwa sheria inaturuhusu hivyo.

“Kwa makosa hayo mawili yaliyokuwa yanamkabili, kamati imemkuta na hatia na kutoa adhabu, kosa la ubaguzi amefungiwa kujihusisha na soka hapa nchini kwa kipindi cha miaka mwili pamoja na faini ya Sh milioni 3, kosa la pili adhabu yake ni faini ya milioni 5,” alisema Mushumbusi.

Mushumbusi alifafanua kuwa licha ya kocha huyo kutimuliwa kazi na waajiri wake lakini watahakikisha faini hizo hazikwepi kuzilipa, njia watakayoitumia ni muhtasari wa maamuzi ya kamati hiyo kuwasilishwa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa).

“Muhtasari wa kikao utaenda Fifa, taarifa zikishafika huko itatambulika adhabu zinazomkabili, hivyo faini atailipa bila ya wasiwasi wowote,” alieleza Mushumbusi.

Chanzo: habarileo.co.tz