Wakati wadau mbalimbali wakiendelea kumsaidia aliyekuwa mshambuliaji wa Polisi Tanzania, Gerrard Mdamu, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), nalo limeibuka kumuokoa jahazi la matibabu ya mchezaji huyo.
Mdamu alipatwa na ajali ya gari, Julai 2021 wakati akitoka mazoezi na timu huyo ilipokuwa Ligi Kuu Bara na kufanyiwa upasuaji ambao umemfanya awe nje ya uwanja kwa mwaka wa tatu sasa kabla ya Mwanaspoti kuimuibukia nyumbani kwake kumjulia hali na kumkuta mambo yakiwa bado kiafya.
Mara baada ya habari za Mdamu kuwa anaendelea kuteseka na kuhitaji msaada, wadau mbalimbali wamekuwa wakijitokeza kumpiga tafu, ikiwamo Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji na nwengine kabla ya TFF nayo kujitosa baada ya Rais Wallace Karia kuiagiza familia ya mchezaji huyo wa zamani wa Mwadui kumpeleka Mdamu Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo gharama za matibabu hayo yatalipwa na shirikisho hilo.
"Hongereni kwa kazi nzuri, mnayofanya, hatukuwa tunafahamu kwamba bado anauhitaji wa matibabu, lakini naomba apelekwe Muhimbili, na gharama za matibabu yake iletwe invoice TFF tutalipa," imesema taarifa ya Karia akizungumza na Mwanaspoti.
Mdamu ameeleza amekuwa akaishi kwa maumivu makali yaliyopo mguu wake wa kulia kiasi cha kumnyima raha hasa kutokana na kutoa usaha na daktari aliyemfanyia upasuaji huo wa awali kutoka Taasisi ya tiba ya mifupa na ubongo Muhimbili (MOI), Dk Kennedy Nchimbi kuagiza aende kuonana naye ili amchunguze.
Mara baada ya mchezaji huyo kuonana na daktari huyo jana, alizungumza na naye na kumfahamika juu ya ukweli kwamba hatacheza tena soka na Mdamu amekubali matokeo.
Kwa taarifa zaidi juu ya alichozungumza Dk Nchimbi na Mdamu fuatilia katika tovuti hii na mitandao ya kijamii ya Mwanaspoti na Mwananchi Communictions Ltd (MCL) kwa ujumla bila kusahau kesho gazetini.