Wakati taarifa ya kutokulipwa kwa wachezaji wa timu ya Taifa ya chini ya miaka 15 ikisambaa mitandaoni Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limesema bado lipo kwenye utaratibu wa kubadili hundi ili ipate fedha.
Taarifa iliyosambaa mtandaoni inaeleza kuwa timu hiyo ilimaliza nafasi ya pili katika michuano ya Caf African Schools Football championship kanda ya Cecafa waliyoshiriki na kupatiwa zawadi ya Sh188.62 milioni huku wachezaji wakipatiwa Sh20,000 ya nauli.
Pia taarifa hiyo inayozunguka mtandaoni inaeleza kuwa wachezaji hao waliachwa mkaoni Tanga na kupokonywa jezi huku wakieleza kuwa jambo hilo ni mara ya pili kutokea ikiwa ni baada ya kumalizika kwa michuano iliyofanyika nchini Uganda waliposhika nafasi ya tatu lakini walipewa Sh50,000.
Akizungumza nasi, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo amesema kila kitu kina utaratibu wake hususani katika kutoa zawadi za mashindano.
"Wamekuwa washindi wa pili na zawadi yao ilitolewa kwa hundi hivyo haiwezekani mashindano yaishe siku chache tu leo hii wawe wamepata hizo pesa kila mtu anajua mambo ya hundi," amesema Ndimbo.