Dar es Salaam. Yanga inalisubiri Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuona ratiba mpya ya Kombe la Azam ili kujipanga na mchezo wao dhidi ya Tanzania Prisons.
Prisons na Yanga zilipangwa kucheza mchezo wao, Aprili 4, lakini kutokana na msiba wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli zilitangazwa siku 21 za maombolezo, huku kukiwa hakuna shughuli nyingine yoyote kuendelea.
Akizungumza jana, Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema timu hiyo ilikuwa na ratiba ya kuweka kambi mkoani Katavi, lakini wamelazimika kusubiri ili kuona ratiba mpya itakayotolewa.
“Shughuli zote zimesimama tunaomboleza msiba kwahiyo hauwezi ukasema unaenda kuweka kambi Katavi huku kukiwa hakuna kitu kinachoendelea, pia ratiba kuna uwezekano ikabadilika kwa sababu mpaka labda tarehe nane siku hizo ndio zitakuwa zimekamilika”.
Akizungumzia upande wa kurejea kambini Avic Town baada ya awali kutoka kwa ajili ya kwenda kutoa salamu za mwisho katika uwanja wa Uhuru, Bumbuli alisema timu yao itarejea kambini Ijuma.
Bumbuli alisema kambi hiyo itakuwa ni maandalizi ya mechi za kombe la Azam pamoja na Ligi Kuu ili kuwafanya wachezaji wawe na utayari wa mwili.