Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TFF wazibane Simba, Yanga kuhusu viwanja

Uwanja Wa Mkapa 1140x640 Uwanja wa Benjamin Mkapa

Tue, 11 Apr 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Taarifa inaonyesha baadaye mwezi ujao Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam unaweza kufungwa rasmi kupisha matengenezo kwa ajili ya mashindano ya Super 8 ambayo Simba inashiriki.

Huu ni kati ya viwanja ambavyo Chama cha Soka Afrika Caf kiliupitisha utatumika kwa michuano hiyo, lakini wataalam waliotumwa wakatoa angalizo la sehemu ambazo zinatakiwa kufanyiwa marekebisho na tayari imeonekana jambo hilo linaweza kufanyika hivi karibuni.

Hili ni jambo zuri kwa kuwa ni maboresho ambayo yataufanya uwanja huo kuwa bora zaidi kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, pia kwa michuano ya kimataifa msimu ujao.

Lakini pamoja na jambo hilo inaonekana sasa uwanja huo umeanza kuelemewa kutokana na kuwa na matumizi ya timu nyingi kwa msimu huu na unawezekana ukatumika zaidi msimu ujao baada ya kuingia kwa timu nne tena kwenye michuano ya Afrika.

Tunaamini sasa umefika wakati wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), pamoja na Bodi ya Ligi kusimama vizuri na kuhakikisha kila timu inakuwa na uwanja wake unaokidhi vigezo vinavyotakiwa badala ya kila moja kufikiri kuhusu Uwanja wa Mkapa tu.

Tumesikia mara kwa mara kuhusu timu za Simba na Yanga ambazo zimekuwa zikishiriki michuano ya kimataifa mara nyingi hapa nchini zinafanya utaratibu wa kujenga viwanja vyao.

Siyo mara moja wala mara mbili tumeona ramani ambazo zimekuwa zikiletwa mbele ya waandishi wa habari wakielezwa uwanja wa Yanga utakuwa kwenye mwenekano fulani na uwanja wa Simba utakuwa kwenye picha fulani lakini jambo hilo limekuwa halifanyiki.

Simba wamewahi kuibuka na kuzungumza kuhusu kujenga uwanja wao kwenye eneo lao la Bunju jijini Dar es Salaam, lakini Yanga wamekuwa wakifanya hivyo na kuzungumza kuhusu eneo la Kigamboni na wakati mwingine Jangwani sehemu ambayo ndiyo makao yao makuu, lakini baada ya muda mambo hayo yamekuwa yakiyeyuka na hakuna jambo ambalo limekuwa likifanikiwa.

Timu mbalimbali zimekuja kwenye soka hivi karibuni na kufanya vizuri zikiwa na viwanja vyao, ukitazama kwa sasa unaona timu za Simba na Yanga zinakwenda kulipa fedha ili kuutumia Uwanja wa Azam Complex ambao unatumia na timu changa ya Azam.

Pia tunaona timu ya Namungo nayo ikiwa na uwanja wa kisasa pamoja na kuja kwenye soka hivi karibuni na baada ya muda tutaona Simba na Yanga zikilipa pia fedha kuutumia uwanja wao kwenye michuano ya kimataifa.

Tunaamini umefika muda sasa wa Simba na Yanga kuhakikisha wanakuwa na viwanja vyao ili wakati mwingine kuupumzisha ule wa Mkapa, kwa kuwa tunaamini kama utaendelea kutumika hivi hata kama utafanyiwa marekebisho kila baada ya miezi sita basi hauwezi kudumu kwenye ubora wake.

Ufike muda TFF na Bodi ya Ligi kuja na kanuni inayotaka kila timu kwenye ligi kumiliki uwanja wake mwenyewe unaofaa kutumika kwenye ligi na michuano ya kimataifa.

Chanzo: Mwanaspoti