Ligi Kuu Tanzania Bara imeanza kwa mzunguko wa kwanza kubakiza michezo miwili, huku mwanzo ukionekana kuwa mzuri japo kuna changamoto bado.
Hii ni ligi namba tano kwa ubora Afrika, ambayo imekuwa bora zaidi msimu uliopita licha ya kuwa na kasoro ndogo ambazo hata hivyo bado zinaendelewa kufanyiwa kazi.
Ligi yetu kuwa bora ilikuwa na sababu nyingi zilizochangia kufika hapo, ikiwamo usimamizi wake, utawala bora wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na usimamizi wa Bodi ya Ligi (TPLB).
Ukiachana na TPLB na TFF, kuna mchango mkubwa wa udhamini wa Ligi Kuu uliopo sasa, ukianzia ule wa haki za matangazo wa Azam Media na mdhamini mkuu, Benki ya NBC.
Yote haya kwa pamoja yanafanya timu kuongeza ushindani na kutoa kitu zaidi uwanjani, jambo ambalo limeonyesha kuwa linaweza kuifikisha ligi hii mbali zaidi ya tunavyodhani aua tulivyozoea.
Hili linatakiwa kulindwa zaidi ya hapa, linatakiwa kuheshimiwa na kutafuta sababu nyingine chanya za kuifanya Ligi Kuu kuzidi kuonekana bora kila uchwao kwa kuongeza bidii katika kilicho bora.
Lakini baada ya mafanikio ya kushika nafasi ya tano, inaonekana kama tunataka kujisahau kwa mambo ambayo hayana udogo wa kuyadharau na kuona kama si sehemu ya ubora wa ligi hii.
Tukio la Kitayosce ni moja ya mambo ambayo yanaweza kuturudisha nyuma katika mbio zetu za ubora kwa mashindano haya makubwa nchini, halikutakiwa kuchukuliwa kwa udogo kama wengi wanavyodhani.
Iwe kwa Kitayosce wenyewe kuwa na makosa ya kusababisha waingie uwanjani wachezaji nane au kwa TFF, suala hili halikutakiwa kuruka katika runinga zetu, ambazo tunajua Azam Media inatazamwa katika nchi nyingi.
Lakini jingine lililoibuka ni suala la mikataba binafsi ya wadhamini wa wachezaji, ambao hawatakiwi kuwa mpinzani wa mdhamini mkuu wa ligi, NBC.
Hili ni tatizo jingine ambalo linakwenda kuweka tofauti kama halitachukuliwa kwa uzito. Kipengele cha mkataba wa sasa wa NBC kimeongezwa na hakikuwepo kwa msimu uliopita, ambao baadhi ya wachezaji wa Simba na Yanga walishakuwa na mikataba na benki nyingine.
Kipengele hiki kimekuja sasa baada ya kuona wachezaji hawa wakiwa na maisha kwingine. Hili linazungumzika bila kuanza kuvutana kwani kipengele hiki kimekuja wakati wachezaji hawa wakiwa tayari na mikataba.
Tunaamini kuwa TFF ilikutana na wajumbe katika kupitia upya kanuni za Ligi Kuu na inaaminika pia kuwa kuna baadhi ya wajumbe walikikataa kipengele hiki, hivyo bado kuna uwanja wa kurudi mezani.
Tunajua kuwa wadhamini wanatakiwa kuheshimiwa, lakini pia tufahamu kuwa kuna maisha binafsi ya wachezaji wetu, hakuna anayependa wachezaji hawa kuwa ombaomba baada ya kumaliza muda wao wa kucheza soka.
Haya na mengine ni miongoni mwa sehemu ambazo zinatupa heshima kubwa kwa kuwa na kupanda kwa ligi yetu, ambayo sasa imeanza kuchukua hata wachezaji kutoka kwenye ligi kubwa kama za Afrika Kusini.