Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TFF kumuenzi Magufuli

E9b061ef9495aaf05e1aab4adced3994 TFF kumuenzi Magufuli

Mon, 22 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limesema litamuenzi Rais John Magufuli daima kwa sababu katika kipindi cha uongozi wake ndiyo wakati timu zote za Taifa zilifuzu kwenye mashindano ya Afrika.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa TFF Kidao Wilfred alipozungumza na gazeti hili jana kuhusu kifo cha Rais Magufuli kilichotokea Jumatano ya wiki hii kutokana na maradhi ya moyo.

Kidao alisema Rais Magufuli licha ya kuwa mwana michezo kwa vitendo na kushuhudia mechi za timu ya Taifa ndio wakati timu za taifa zilianza kufanya vizuri na kufuzu mashindano ya Afrika.

Alisema walianza na Taifa Stars kufuzu Afcon baada ya kufanya hivyo baada ya miaka 39, pia ikafuzu Chan, timu ya soka la ufukweni nayo ikafuzu, U17 imefuzu mara mbili na U20.

“Kwanza ilifuzu Taifa Stars, akawaita ikulu na kuwapongeza na kuwazawadia viwanja kila mchezo, Taifa Stars ya wachezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan) nayo ilifuzu, timu ya U-17 imefuzu mara mbili na U-20 imefuzu kwa mara ya kwanza pia timu ya soka la ufukweni nayo ilifuzu,”

“Kwetu sisi ni historia ambayo itatufanya tuendelee kumkumbuka Rais Magufuli kwani pia aliwatambua wachezaji waliotoa jasho kutetea bendera ya Tanzania kwa kuwapa viwanja vya kujenga nyumba ambavyo vipo Dodoma karibu na mji wa serikali, Mtumba,” alisema Kidao.

Pia Kidao alisema watamuenzi daima kwani pia alitoa Sh bilioni 1 kwa ajili ya kuandaa fainali za vijana za Afrika na kufanya Tanzania kupata sifa, kwani zilifana sana.

“Wakati alipoita wachezaji wa Taifa Stars Ikulu kuwapongeza ndipo alipotoa Sh bilioni 1 kwa ajili ya kusaidia maandalizi ya fainali za vijana zilizofanyika hapa nchini, ukweli serikali ilifanya fainali hizo kuwa kati ya fainali bora kutokea za Shirikisho la Soka Afrika (Caf), “ alisema Kidao.

Aidha, alisema licha ya kufanya vizuri kimataifa pia ligi ya soka ya Tanzania Bara mwaka huu imeiingia katika rekodi ya ligi bora nane Afrika na msimu wa mwaka juzi waliingiza timu nne kwenye mashindano ya Caf.

“Katika uongozi wake tuliingiza timu nne kwenye mashindano ya Afrika kwa maana ya timu mbili Ligi ya Mabingwa Afrika na timu mbili Kombe la Shirikisho na Ligi Kuu Tanzania Bara imekuwa ligi ya nane kwa ubora Afrika,” alisema Kidao.

Kidao alisema Rais Magufuli atakumbukwa kwa hotuba yake ya mwisho akizindua Bunge mwishoni mwa mwaka jana baada ya uchaguzi kuhusu uwekezaji mkubwa katika michezo.

“Tutamuenzi kwa kuhakikisha tunasimamia vizuri rasilimali za mpira wa miguu na kusimamia vizuri shughuli zote za mpira wa miguu na kuongeza ajira kama alivyoamini katika kutengeneza viwanda ili kuongeza ajira.

Chanzo: www.habarileo.co.tz