Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TFF ianze mikakati matumizi ya VAR katika Ligi Kuu

Var Pic TFF ianze mikakati matumizi ya VAR katika Ligi Kuu

Wed, 31 Aug 2022 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa sasa imesimama ili kuiwezesha timu ya soka ya Taifa (Taifa Stars) kucheza mechi za kutafuta tiketi ya kufuzu kwa ajili ya mashindano ya wachezaji wanaocheza katika ardhi za nchi zao (Chan)yaliyopangwa kufanyika nchini Algeria mwakani mwanzoni.

Stars ilicheza na Uganda juzi Jumapili na kupoteza kwa bao 1-0 nyumbani. Mchezo wa pili wa timu hizo utachezwa Septemba 3 nchini Uganda.

Katika Ligi Kuu mpaka sasa kila timu imecheza mechi mbili huku timu tatu - Yanga, Simba na Singida Big Star hazijapoteza hata mechi moja.

Kwa maana hiyo, timu hizo zote zimejikusanyia pointi sita na Simba inaongoza ligi ikiwa na uwiano mzuri wa mabao - matano - kwani haijaruhusu hata bao moja mpaka sasa.

Yanga ipo katika nafasi ya pili na Singida Big Stars ikishika nafasi ya tatu.

Mpaka sasa mechi 33 (pamoja na ile ya Ngao ya Jamii iliyozikutanisha Yanga na Simba) huku mechi za Ligi Kuu pekee (yaani mechi 32) mpaka sasa zimevuna jumla ya mabao 40, huku kila mzunguko ukivuna mabao 20 kila mmoja.

Mbali na mabao, kumekuwa na matukio mengine kama ya wachezaji kuonyeshwa kadi nyekundu, kadi za njano, penalti na maonyo mbalimbali kwa wachezaji na makocha.

Pia, kumekuwa na malalamiko yasiyo rasmi kwa waamuzi ambayo yametawala huku mashabiki wakipaza sauti ikiwa ndiyo kwanza ligi hiyo ipo katika hatua za awali kabisa. Hoja nyingi za mashabiki wa soka zimeelekezwa kwa mamlaka yaani - TFF na kamati zake mbalimbali na Bodi ya Ligi (TPLB).

Hali hiyo imesababisha mashabiki kuzilalamikia mamlaka kwa kutochukua hatua kwa mujibu wa kanuni za kusimamia na uendeshaji wa Ligi Kuu.

Moja kati ya matukio ambayo yamekuwa gumzo kubwa ni tukio la rafu lililomhusha beki Henock Inonga wa Simba dhidi ya Salum Aboubakary ‘Sure Boy’ wa Yanga, Mtenje Albano wa Coastal Union dhidi ya Yannick Bangala wa Yanga na beki mwingine wa Coastal Unio,n Lameck Lawi dhidi ya Jesus Moloko wa Yanga. Kuna matukio mengi zaidi ya hayo niliyoyataja ambayo yametokea katika mechi 32 za Ligi Kuu na Ngao ya Jamii.

Ni wazi kuwa pamoja na waamuzi kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kuwaadhibu wahusika kwa kadi za njano na nyekundu, bado kuna mashabiki wanaamini kuwa bado adhabu hizo hazitoshi kutokana na aina ya matukio yaliyotokea.

NINI CHA KUFANYA

Ni wazi kuwa utatuzi mkubwa wa matukio (malalamiko) haya ni kuwekeza kwenye teknolojia ya kusaidia uamuzi wa soka (VAR) pamoja na kuwa ni gharama kubwa.

Inawezekana kuwa baadhi ya matukio yameamualiwa zaidi ya adhabu na mwamuzi au chini ya kanuni na mengine hayakuchukuliwa hatua zozote kutokana na kukosekana kwa teknolojia hiyo.

Ni ukweli usiopingika kwamba VAR ina changamoto zake ambazo baadhi ya nchi ambazo zinaitumia zimekutana nazo.

Bado kwa soka la Tanzania VAR inaweza kusaidia kuondoa au kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto na malalamiko ambayo ni ya kawaida sana na kuifanya ligi kuwa bora zaidi ya ilivyo hivi sasa katika mechi za mashindano mbalimbali.

Wiki kadhaa zilizopita, TFF kwa kushirikiana na Televisheni ya Azam walifanya majaribio ya matumizi ya VAR katika mechi za wachezaji walio chini ya miaka 20 na kuona ufanisi wake.

Matumizi ya teknolojia hiyo yalileta ufanisi mkubwa katika mashindano na tuliweza kushuhudia maamuzi mengi yakibatilishwa kutokana na picha za marejeo ambapo mwamuzi alikwenda kujiridhisha. Ni ukweli usiopingika kuwa kuna changamoto ya miundo mbinu mbali ya gharama kubwa za uwekezaji wa teknolojia hiyo, lakini naamini VAR ya Azam TV haina gharama kubwa kulinganisha na ambayo Shirikisho la Kimataifa la Vyama va Soka (FIFA) imeipitisha, hivyo kinachotakiwa ni ‘kuwaomba’ wahusika kuruhusu matumizi ya VAR iliyotokana na ubunifu wa Watanzania.

Pia, Serikali ilitangaza katika moja ya vikao vyake vya Bunge la Bajeti uwezekano wa kutumia teknolojia hiyo ambayo ipo chini ya Bodi ya Kutunga Sheria za Soka Duniani, IFAB ambapo gharama zake si chini ya Sh 14 bilioni.

Inawezekana kuwa kuna ‘utaratibu’ ambao FIFA wameuweka ili kufanikisha matumizi ya VAR kwa nchi ambayo zinahitaji matumizi ya teknolojia hiyo, lakini bado taratibu hizo si ‘kikwazo’ kulingana na uwekezaji katika ligi yetu mpaka sasa.

Ni wazi kuwa kwa mwelekeo wa ligi yetu, uwekezaji uliokuwepo na umaarufu katika barala Afrika, TFF na TPLB ianze mikakati ya kufanikisha matumizi ya teknolojia hiyo na kuendelea kuleta maendeleo ya soka nchini.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz