Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa tamko juu ya sakata la vilabu kufungiwa kusajili ambapo imesisitiza kuwa klabu zikifungiwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kusajili wachezaji, zitafunguliwa na shirikisho hilo pekee na si vinginevyo.
Taarifa ya TFF ya leo Juni 19, 2024 imebainisha kuwa kwa mujibu wa utaratibu wa FIFA, mdai anatakiwa kuthibitisha kupokea malipo ndani ya siku tano baada ya mdaiwa kufanya malipo husika. Iwapo mdai atathibisha kupokea malipo yake, ndipo FIFA itaiondolea klabu husika adhabu ya kufungiwa kusajili.
“TFF itaendelea kutoa taarifa kuhusu klabu zote zilizofungiwa na FIFA kufanya usajili wa wachezaji kutokana na kudaiwa. Pia itaendelea kutoa taarifa kuhusu zile ambazo zitakuwa tayari zimefunguliwa na FIFA baada ya kuwalipa wahusika.” — TFF