Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

TBT: Aden Rage hatolisahau hili tukio, alilia kama mtoto

Yanga Twite WA001 Aden Rage hatolisahau hili tukio, alimwaga machozi kama mtoto

Thu, 29 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwaka 2012 wakati Klabu ya Simba wakiamini wameshinda vita ya kupata saini ya nyota wa APR ya Rwanda wakati huo, Mbuyu Eric Gasana Twite, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Kimataifa ya Yanga SC, Seif Ahmed 'Magari' alifanya umafia ambao Mwenyekiti wa Simba wakati huo Aden Rage hawezi kuusahau.

Alimuwekea pesa ndefu Mbuyu Twite ambaye alitia kandarasi ya kuichezea timu ya Wananchi Yanga na kuacha kilio kizito viunga vya Msimbazi.

Wakati huu kipindi cha usajili kulikuwa na vita kali sana mitaa ya Kariakoo, mmoja akijua jina la mchezaji unayetaka kumpa kandarasi atapita nae kesho utashangaa yupo upande wa pili hata kama wewe ulikuwa na nafasi kubwa ya kumpata



Mbuyu Twite alikuwa na uwezo mkubwa wa kucheza beki wa pembeni (kulia ) na kiungo wa ulinzi. Haya ni maeneo ambayo alikuwa anakupa kitu bora sana ndani ya Dimba.

Mzee Rage hawezi kusahau kwa sababu alienda kwa mbwembwe Kigali na kumkabidhi fuko la pesa Mbuyu Twite, wakati anaondoka, Yanga wakampandilia, wakampa pesa na mkataba juu kisha kuja nae Dar eS Salaam kibabe kama mfalme.

Rage alidai kuwa mtoto mmoja wa kigogo ndiye alihusika kuwanyang'anya mchezaji huyo na kumpelekea kumwaga chozi sambamba na kujiuzuru nafasi yake ya Ujumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria, Maadili na Hadhi za wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa madai ya shirikisho hilo kuikandamiza klabu yake.

Akijibu tuhuma hizo katika Makao Makuu ya klabu hiyo Mtaa wa Twiga na Jangwani aliyekuwa Katibu Mkuu Yanga, Selestine Mwesigwa alimtaka Rage kumtaja na kuleta vithibitisho juu ya hilo mapema bila ya kuambiwa muda.



Aidha Mwesigwa alitoa ufafanuzi juu ya suala la Mbuyu Twite ambaye Simba walidai kumsajili, Yanga walimsajili kwa kufuata na kuheshimu kanuni na sheria za CAF, TFF na FIFA hivyo basi wao hawajakurupuka katika usajili wake.

Alisema wao walianza kufanya mchakato wa kumnasa beki huyo toka Novemba 2011, kabla ya kuanza mazungumzo na Simba juu ya aliyekuwa beki wao Kelvin Yondan na kusema kuwa walimtuma Mjumbe wa kamati ya Utendaji Abdallah Binkrebu kumfuatilia toka kipindi hicho.

Binkrebu akafunga safari na kwenda kuzungumza na uongozi wa timu yake ya Fc Lupopo ya Congo DR na wala sio APR, Simba wao walinunua mali ya wizi wakati Yanga wakisema walikwenda kwa mwenye mali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live
Related Articles: