Kiungo na mkongwe wa KMC Mugiraneza Jean Baptist 'Migi' amepata pigo baada ya kufiwa na mama yake mzazi.
Mama wa Migi Pascasie Bandirimbako amefariki jijini Kigali jana baada ya kuugua kwa muda mfupi katika Hospitali ya Rufaa ya Taifa CHUK.
Taarifa kutoka Rwanda zinasema ratiba ya mazishi hayo yatafanyika Alhamisi akisubiriwa Migi ambaye ataondoka nchini leo kurudi kwao Rwanda.
Msemaji wa KMC Christina Mwagala amethibitisha kutokea kwa msiba huo akisema tayari klabu hiyo imeshamuandalia taratibu za safari kiungo huyo.
"Klabu imepokea taarifa hiyo ya simanzi kwa kiungo wetu Migi kufiwa na mama yake na ataondoka nchini leo kwenda kwao kwa taratibu za mazishi," amesema Mwagala.
Aidha ratiba hiyo inaonyesha kuwa mazishi hayo yatafanyika katika Makaburi ya Nyamirambo jijini Kigali.