Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sven kubariki ubingwa Mbeya

95095 Sven+pic Sven kubariki ubingwa Mbeya

Mon, 22 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

IKIWA imebakisha pointi 10 ili kujihakikishia kutetea taji la Ligi Kuu Tanzania Bara, Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, amesema anahitaji kutangaza ubingwa wa msimu huu wakiwa jijini Mbeya, imeelezwa.

Simba itatua Mbeya ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 3-0, walioupata dhidi ya Mwadui FC, shukrani kwa mabao yaliyofungwa na Hassan Dilunga, John Bocco na Agustino Simon, ambaye alijifunga katika harakati za kuokoa shambulizi langoni mwake.

Vinara hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara wanatarajia kusafiri kuwafuata Tanzania Prisons na Mbeya City, katika mechi mbili mfululizo zitakazochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine kati ya Juni 24 na 28, mwaka huu.

Akizungumza na gazeti hili, Sven aliwapongeza wachezaji wake kwa ushindi waliopata dhidi ya Mwadui FC na kuwaeleza anahitaji kuona wanajituma na kujitolea katika michezo inayofuata ili kutangaza ubingwa mapema.

Sven alisema malengo yake ni kutangaza ubingwa mapema kabla ya kurejea jijini Dar es Salaam kukutana na Azam FC katika mechi ya hatua ya robo fainali ya mashindano ya Kombe la FA.

"Wachezaji wangu wanatakiwa kujituma zaidi, katika michezo yetu ikiwamo dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons, kucheza kama ilivyocheza dhidi ya Mwadui, ili kutangaza ubingwa mapema. Ingawa najua haitakuwa rahisi," Sven alisema.

Alisema baada ya hapo watakutana na mechi zenye ushindani kwa sababu kila upande utashuka uwanjani ukiwa na malengo tofauti kwenye Ligi Kuu na mashindano hayo ya Kombe la FA.

"Mwezi ujao tutakapotoka Mbeya, tutakutana na mechi ya ushindani mkubwa, ni robo fainali ya Kombe la FA, ni mechi nzuri, pia ngumu kwa timu zote," alisema Sven.

Aliongeza amefurahishwa kuona wachezaji wake wamefanikiwa kushika mabadiliko ya mfumo wa uchezaji kwa haraka ndani ya siku tatu na kufanya vema na hatimaye kupata ushindi mnono.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live