Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sven awafagilia nyota wake

0eb96f231ed8a142e6553ddbfe257997.jpeg Sven awafagilia nyota wake

Mon, 28 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KOCHA wa Simba, Sven Vandenbroeck, amefagilia kiwango kilichooneshwa na wachezaji wake kwenye michezo miwili mfululizo ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Biashara United na Gwambina, iliyofanyika kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.

Sven ametoa pongezi hizo kwa kikosi chake wakati anafanya tathimini baada ya timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Gwambina FC, matokeo yanayowafanya kushika nafasi ya pili kwenye msimamo baada ya kufikisha pointi 10 na wamefunga mabao 10 katika michezo minne waliyocheza.

Alisema mchezo huo ulikuwa mgumu kutokana na ubora wa wapinzani wao katika utimamu wa miili, lakini wachezaji wake walijitahidi kupambana kwa nguvu kutafuta ushindi.

“Nawapongeza wachezaji wangu kwa kufanya vizuri kazi yao wanayopaswa kutimiza, wamepambana, wametengeneza nafasi na kupata ushindi, kwa ujumla nimeridhishwa na kiwango walichoonesha kwenye michezo miwili nikianza na Biashara tulioshinda mabao 4-0 na dhidi ya Gwambina,” alisema.

Alisema kikosi chake mwishoni mwa wiki kitaenda kucheza ugenini jijini Dodoma dhidi ya JKT Tanzania na wanategemea kuendeleza makali yao waliyoyaonesha katika mechi mbili zilizopita, ambapo wamefunga jumla ya mabao saba.

Alisema ushindi unadhihirisha jinsi kikosi chake kilivyo na uchu wa kutafuta ushindi.

Pia Sven alisema kwenye mchezo dhidi ya Gwambina FC alifurahishwa zaidi na kitendo cha kikosi chake kupata mabao mawili kati ya matatu waliyofunga kupitia mipira iliyokufa, ambapo katika mchezo huo Simba walipata bao la kwanza kupitia Meddie Kagere kwa njia ya kichwa akiunganisha mpira wa kona uliopigwa na Luis Miquissone na la pili la Pascal Wawa kwa mkwaju wa adhabu.

“Kwa mara ya kwanza naona wachezaji wangu wanapata mabao kwa kutumia vema mipira iliyokufa, ni vitu ambavyo unategemea kwa timu yeyote kwa wachezaji waliodhamiria kutafuta ushindi,” alisema Sven.

Alisema kwakuwa hawakupata kipindi kirefu cha maandalizi ya msimu, anatumia michezo ya ligi kuwaandaa wachezaji wake kwa ajili ya kutengeneza kikosi bora na chenye ushindani kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika mchezo huo, mabao ya Simba yalifungwa na Kagere, Wawa na mshambuliaji mpya Chris Mugalu anayeonekana kuonesha makali siku zinavyozidi kusonga mbele, ambapo tangu ajiunge na Simba amecheza mechi nne na kufunga mabao manne.

Chanzo: habarileo.co.tz