Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sven ajivunia ven ajivunia kikosi chake

16e3cfc17f757ca16d04f2962c5ba50b Sven ajivunia ven ajivunia kikosi chake

Wed, 9 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KOCHA wa Simba, Sven Vandenbroeck, amesema upana wa kikosi chake utamsaidia kupanga wachezaji kwa kuzingatia mazingira ya uwanja watakaokwenda kucheza mikoani.

Sven alitoa kauli hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ihefu FC katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliofanyika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, Mbeya, wiki iliyopita.

Akizungumza Dar es Salaam juzi, Sven alisema viwanja vingi vinavyotumika kwenye michezo ya ligi havina ubora unaomfanya mchezaji kuonesha uwezo wake, ila anashukuru kuwa na kikosi kipana.

“Nina hazina ya upana wa kikosi kitakachonisaidia kupanga wachezaji kulingana na mazingira ya uwanja tunaokwenda kuutumia kwenye kila mchezo wa ligi,” alisema Sven.

Alisema anajua mchezo unaokuja na Mtibwa Sugar uwanja watakaotumia wa Jamhuri Morogoro hauna tofauti na waliotoka kucheza dhidi ya Ihefu FC. “Mashabiki wategemee kuona mabadiliko makubwa ya wachezaji karibia kila mechi kwa kuwa lengo letu ni kutafuta ushindi kwenye kila mchezo ili kuhakikisha tunatetea ubingwa kwa mara ya nne mfufulizo,” alisema.

Sven alisema ili wafanikiwe kutetea ubingwa wa ligi, kila mchezo wanatakiwa kuibuka na ushindi, matokeo yatakayoanza kuwajenga waweze kushindana mchezo unaofuata.

Kikosi cha mabingwa hao baada ya kuwasili Dar es Salaam kutoka Mbeya, jana kiliingia kambini kuanza mazoezi ya kukabiliana na Mtibwa Sugar unaotarajiwa kuchezwa Jumamosi ijayo.

Baada ya michezo ya mzunguko wa kwanza, Simba inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi tatu sawa na KMC inayoongoza kwa wingi wa mabao ya kufunga.

Azam inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi tatu sawa na Biashara United, Dodoma Jiji, JKT Tanzania na Namungo FC.

Chanzo: habarileo.co.tz