Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sven: Wachezaji Simba wanarejesha viwango

SIMBA YA KWELI.webp Sven: Wachezaji Simba wanarejesha viwango

Mon, 8 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

KOCHA Mkuu wa Simba, Mbelgiji Sven Vandenbroeck, amesema kwa sasa wachezaji wake wameanza kurejea kwenye viwango vyao vya kawaida, baada ya mazoezi ya siku 12 sasa.

Kocha huyo alikuwa akizungumzia kiufundi juu ya maandalizi ya kikosi hicho kilichoanza kujiandaa na mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, pamoja na Kombe la FA kuanzia Mei 27, mwaka huu.

Sven baada ya michezo kusimama tangu Machi 17, mwaka huu kutokana na kuibuka mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19, unaosababishwa na virusi vya corona, alianza kukinoa tena kikosi hicho Mei 27, baada ya serikali kuruhusu tena michezo kuendelea nchini.

Alisema pamoja na kuwapa maagizo ya kufanya mazoezi nyumbani, lakini hawakuwa fiti kwa asilimia zote, hivyo kitu cha kwanza alichoanza nacho ni kuwarejeshea utimamu wa mwili.

"Tulikuwa na siku nne za kurudisha utimamu wao wa mwili ili wawe fiti, halafu baada ya hapo tukaja na siku kadhaa za kuwarejeshea uwezo wa kupambana mmoja mmoja na baada ya hapo siku hizi zilizobaki, tunachofanya ni kuwafundisha wachezaji mbinu za kimpira," alisema kocha huyo.

Jumapili ijayo kocha huyo atakuwa kwenye kibarua cha kwanza baada ya corona, Simba itakapopambana dhidi ya Ruvu Shooting kwenye mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Sven ana mechi tano ya kuiwezesha Simba kutwaa ubingwa mara tatu mfululizo na kuingia kwenye vitabu vya kumbukumbu ya makocha walioiwezesha timu hiyo kongwe kufanya hivyo.

Kama Simba itatwaa ubingwa ambao utakuwa ni mara ya tatu mfululizo, yeye mwenyewe itakuwa ni mara ya kwanza kuiwezesha timu hiyo kuchukua ubingwa, kwani msimu wa 2017/18 ilipotwaa ilikuwa chini ya kocha Mfaransa Pierre Lechantre, msimu wa 2018/19, ilitwaa chini ya Mbelgiji Patrick Aussems.

Sven anaweza kuwapiku makocha hao kama Simba itatwaa pia Kombe la FA, kwani chini ya makocha hao, timu hiyo iliondolewa mapema kwenye michuano hiyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live