Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sure Boy ana rekodi yake CAF

Sure Boy PP Kiungo wa Yanga, Sure Boy

Wed, 8 Mar 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Mashabiki wa soka wanamuita ‘Babu Kaju’ wakivutiwa na umahiri wake wa kupiga pasi nyingi tangu akiwa Azam FC kabla ya kutua Yanga na kuthibitisha ufundi wake, kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ amekimbiza mbaya hadi kwenye michuano ya CAF.

Sure Boy, mtoto wa nyota wa zamani wa kimataifa wa Yanga aliyewahi kutamba na Sigara, Tanzania Stars na Kajumulo World Soccer na Taifa Stars, ametajwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kama kinara wa Yanga wa pasi katika mechi za makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku mwenyewe akifunguk alivyopania makubwa zaidi.

Nyota huyo anashika nafasi ya tatu kwa kupiga pasi 82 akitanguliwa na Mohamed Hrimat wa FAR Rabat ya Morocco mwenye pasi 86, huku kinara akiwa ni Hatim Essaouabi pia wa FAR Rabat aliyepiga 92 katika mechi za raundi tatu za michuano hiyo.

Rabat ipo Kundi C na Yanga ikiwa Kundi D na kesho itashuka Kwa Mkapa kuivaa Real Bamako ya Mali iliyotoka nayo sare ya 1-1 wiki iliyopita jijini Bamako.

Akizungumza na Mwanaspoti kutokana na takwimu hizo, Sure Boy alisema zimemuongezea morali ya kujituma ili kuhakikisha anasaka rekodi zaidi CAF na kubwa zaidi anatamani Yanga ifike mbali.

“Kila mchezaji yupo kwa ajili ya Yanga kadri tunavyopambana kuisaidia timu na rekodi za mchezaji mmoja mmoja zinatokea humo kulingana na kiwango anachokionyesha. Ndio maana nasisitiza timu kwanza mengine yatakuja yenyewe,” alisema Sure Boy.

“Kila mchezaji ana mchango wake kwenye timu kama mimi nimepiga pasi nyingi wapo waliolinda timu isifungwe, wengine wamefunga mabao, waliotoa asisti, kikubwa ni kuijenga Yanga imara yenye ushindani dhidi ya wapinzani wetu.”

Katika michuano hiyo Yanga iliifunga TP Mazembe ya DR Congo mabao 3-1, huku ikipoteza 0-2 kwa US Monastir ya Tunisia na ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Real Bamako na kuifanya ikusanye pointi nne ikishika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi.

Chanzo: Mwanaspoti