Dar es Salaam. Nyota wa zamani wa soka nchini wametaja sababu za mshambuliaji wa Yanga, David Molinga kuwagawa mashabiki wa klabu hiyo licha ya kuendelea kufumania nyavu msimu huu.
Pamoja na kufunga mabao ambayo yamekuwa yakiiwezesha Yanga kuvuna pointi tatu muhimu ikiwamo bao pekee la juzi katika mchezo na Ruvu Shooting, mashabiki wa Yanga wamekuwa na hisia tofauti juu yake ambapo wapo wanaomkubali na wengine kutomwamini.
Akizungumzia kiwango cha Molinga, mshambuliaji wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella alisema sababu ya kutokubalika kwa kiasi kikubwa ni matarajio makubwa ambayo mashabiki wa Yanga waliaminishwa baada ya kuondoka kwa mshambuliaji Heritier Makambo.
“(Molinga) siyo mshambuliaji mbaya, ana uzuri wake ndiyo sababu anaongoza kwa mabao katika kikosi cha Yanga, lakini pia ana udhaifu wake,” alisema.
Mogella alisema mshambuliaji huyo ana akili ya kujua mikimbio ya mpira ndio maana amekuwa anafunga kwani anafahamu kusimama katika nafasi sahihi ingawa siyo aina ya mshambuliaji wa kuamua matokeo.
“Mfano mimi, nilipewa jina la Golden Boy kwa sababu nilikuwa na uwezo huo na nimewahi kubadilisha matokeo. Katika moja ya mechi za Simba mashabiki tayari wakiwa wameanza kuondoka uwanjani wakiamini tumefungwa nikasawazisha, Molinga siyo mchezaji wa aina hiyo.”
Pia Soma
- Ratiba Ligi Kuu pasua kichwa
- Manchester United yampa presha Cantona
- Bayern Munich yamuwekea donge nono Firmino
“Ni kweli anafunga, lakini uwezo wake na kile ambacho mashabiki walikitarajia ni vitu viwili tofauti. Atakuwa amemfikia Makambo kwa asilimia 60, ndiyo maana bado anawapa mashaka mashabiki pamoja na kwamba anafunga,” alisema.
Mayay alisema Molinga ana sifa ya kusimama mahali ambapo mpira utamfikia jambo ambalo sio kila mtu analijua na pia mikimbio yake ni mizuri, ana utulivu na ana uwezo wa kutunza mpira, lakini hawezi kufanya uamuzi wa kujitoa kama alivyokuwa akifanya Makambo, Emmanuel Okwi au hata Mapinduzi Balama kwa sasa.
“Ili awe mzuri zaidi, anahitaji kujitoa, asiwe mchezaji wa kurudisha mipira nyuma anapopewa pasi ili awe salama. Anahitaji pia kujitoa na kulazimisha mabao jambo ambalo Molinga hana, ndio sababu bado hajakubalika kwa mashabiki.”
Beki wa zamani wa Yanga, Fred Minziro alisema mshambuliaji mzuri huonekana kwa tabia za uwanjani hata kama hafungi lakini anavyocheza.
“Mchezaji akiwa mzuri hata mtaani salamu zinasikika, lakini pia hakuna kitu kizuri kwa mchezaji kama kukubalika.Mashabiki wataonyesha mashaka pale utakapokosa kile walichoaminishwa kuwa unacho,” alisema Minziro.