Anaitwa Kelvin Yondani na ukipenda unaweza kumuita ‘Cotton Juice’. Kwa sasa anakiwasha Geita Gold lakini aliwahi kutamba na Simba na Yanga. Nilichokigundua katika muda mfupi niliokaa naye ni mtu wa tofauti sana.
Ni mpole mwenye ucheshi ndani yake na anadhani kuna vitu vingi ambavyo sehemu ya jamii ya wanamichezo humhukumu tofauti na uhalisia wake. Kumbe hayuko hivyo yeye hupuuzia na kuendelea na yale yanayomhusu ndani ya uwanja.
Katika mahojiano yake na Mwanaspoti mkoani Morogoro ambako Geita imeweka kambi kujiandaa na msimu ujao, Yondani anafunguka upande wake wa pili wa maisha yake.
Unadhani kwa nini jamii ya wanamichezo inakuona kauzu? “Ninapoongea na wewe nje ya uwanja unanionaje? Mbona tunacheka muda wote, kauzu huwa anacheka kama hivi? Nadhani hawajanifahamu upande wa pili wa maisha yangu, wamemchukua Yondani wa uwanjani na kumpeleka kwenye maisha ya kawaida.
“Miaka ya nyuma nilikuwa na kampani yangu ambayo ilikuwa ya wahuni sana, walikuwa ni mabraza wanaoujua sana mpira kitu kilichokuwa kimefanya niwe karibu nao ili kujifunza ufundi wao, sasa hata baada ya kuachana nao na kubadilika bado natazamwa vilevile, hicho ndicho kilichoniponza, ila wakisoma makala yako, wakiamua kunielewa watanielewa wakiamua kukomaa na msimamo wao yote nayaona sawa tu,”anasema.
“Laiti wangejua jamii tunayoishi nayo wanavyotuheshimu, wasingepata nguvu kutuona wanavyotuona, jamani sisi ni binadamu kama wao, kama kuna upungufu ni wa kibinadamu na siyo kwa ubaya wa kutuona tumeshindikana ndio maana wengine hatutaki kutumia nguvu kujibu kila jambo,” anasema.
KUMTEMEA MATE ASANTE KWASI
Yondani anakiri kufanya matukio mengi kwenye maisha yake ya soka, mengine yapo wazi kwenye mitandao ya kijamii, ambapo kwa sasa anasema ameacha. Anasema kuna wakati baba yake mzazi (Yondani) alimuweka kitako na kumwambia “Mzee baba, sasa umekuwa unapaswa kuachana na hayo mambo, hebu yapunguze mwanangu, umeyafanya matukio hayo kwa sasa yaache, huwa namuelewa na mimi sioni haja tena.”
Katika matukio hayo analikumbuka la aliyekuwa mchezaji wa Simba, Asante Kwasi alivyomtemea mate usoni Aprili 30, 2018 lilivyomfanya alijutie, ilikuwa mechi ya dabi, Uwanja wa Benjamin Mkapa, tukio hilo lilifanya ashambuliwe mitandaoni na watu kwa kumuona hana ubinadamu.
“Nilichukia sana baada ya kunitukania mama yangu ambaye hakuwepo uwanjani na hahusiki kwa namna yoyote ile, nikawaza yeye mwenyewe kazaliwa na mwanamke, sijui alioa au la, ana dada ama ndugu wa kike, anaanzaje kutoa tusi kama lile tena bila aibu na mchezaji anayepaswa kuigwa na wengine.
“Niliwaza nimfanyie nini ili nimkere kwa kunitukania mama yanga ambaye hajawahi hata kumuona, ndio maana nikamtemea mate na najua alikeleka kama nilivyoumia kwa tusi lake, maana niliona siwezi kuvumilia kila nilipowaza nikawa naiona picha ya mama yangu mbele yangu,” anasema na kuongeza;
“Ninachoshukuru mzee wangu kacheza, hivyo anajua uhuni wa viwanjani, aliponiuliza juu ya hilo, nilipomweleza akanielewa, zaidi alinisisitiza nijitahidi kujizuia inapotokea ishu kama hiyo. Sasa kupitia Mwanaspoti jamii itaelewa upande wangu kujua kilichosababisha nifikie hatua hiyo, najua mechi ilikuwa tafu sana, tulikuwa na bato kali mimi na Kwasi, ila angenitukana mimi na siyo mama yangu.”
TUKIO LA MAYELE
Mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), ambayo Geita Gold ilitolewa kwa mikwaju ya penalti 7-6, Yondani alimchezea rafu aliyekuwa straika wa Yanga, Fiston Mayele na alifungiwa mechi tatu na kulipa faini ya shilingi milioni moja, anafafanua ilivyokuwa.
“Kwa wale ambao waliangalia mchezo huo ulikuwa tafu sana, ndio maana tulifikia hatua ya matuta, sikumkanyaga kwa makusudi kama nilivyoshambuliwa kwenye mitandao ya kijamii, wapo walioandika kwamba mimi ni mchezaji mkubwa lakini nina rafu mbaya, niliamua kunyamaza na kuyapokea yote ndio mpira.
“Mayele ndiye alikuwa hatari kwenye kikosi chao, sasa huku na kule wakati nataka kuokoa hatari kumbe alikuwa nyuma nikamkanyaga kwa bahati mbaya, ila kwasababu wamenizoea mgumu nikahukumiwa.”
ISHU YAKE NA NIYONZIMA
Anafichua urafiki wake ulipoanzia na Haruna Niyonzima wakiwa wanacheza pamoja Yanga, kabla ya kushibana naye anasema alikuwa anashangaa Mnyarwanda huyo anavyopenda kukaa karibu naye na kufuatilia uchezaji wake, akitoka kwenye mechi anamwambia alivyopafomu, iwe vizuri ama vibaya.
“Niyonzima ni mchezaji mkubwa sana, kitendo cha kunifuatilia ninavyocheza, ujue kaona kitu cha tofauti, siku moja alinishangaza akaniambia Yondani nataka tuzungumze vitu vya kimaisha na vya msingi sana, ukimaliza mishe zako nitafute, sikusita baada ya kupata muda sahihi wa kumsikiliza, nikamtafuta,” anasema na kuongeza;
“Akaniambia wewe jamaa unajua kucheza sana, una kipaji kikubwa mno, napenda tuwe ndugu, unaonaje niwachukue watoto wako baadhi wakasome nchini kwetu Rwanda, nikamuona ana upendo sana, pia kasema nakuelewa zaidi ya wengine wanavyokuchukulia tangu hapo nikaanza kumuamini na tumekuwa zaidi ya marafiki;
Anaendelea kusimulia”Familia zetu zinafahamiana, tunasaidiana kwa shida na raha, kiukweli siwezi nikamuelezea Niyonzima nikamaliza hapa, kitu kikubwa mara nyingi anachoniambia anasema usifosi watu wakaamini wewe ni mwema, ipo siku watajua wema wako, amini katika ndoto zako na siyo zao, maana anajua kila mtu ana kusudi lake duniani.
“Ingawa mpango wa watoto kwenda kusoma Rwanda haukufanikiwa, lakini linaweza likatokea lolote mmoja wa vijana wangu kwenda huko, kwani bado analisisitiza hilo, jamaa hana wivu anapoona mwingine anafanikiwa na anamsapoti na kumuongezea maarifa zaidi, ukiachana na huyo mwingine ni Juma Abdul naye alikuwa mshikaji wangu sana Yanga.”
MWILI WAKE
Kiwango chake tangu aanze kucheza Ligi Kuu ni bora, nyuma ya pazia anataja kinachofanya asitoke nje ya ramani ya soka ni nidhamu, kujitambua, mazoezi, vyakula na kuipenda kazi hiyo kwa moyo mmoja.
“Ninapozungumzia nidhamu ni kuanzia muda wa kufanya mazoezi, kula kwa wakati napenda sana vyakula vya kiasili na chakula changu pendwa sana ni dagaa na ugali, kupumzika kwa wakati, sikimbizani na starehe ambazo nimewaachia vijana bwana,”anasema na kuongeza;
“Nimejipambanua, kwani mimi ni baba, watoto wangu wanasoma kupitia mpira naanzaje kuukosea adabu, ukiachana na hilo kadiri siku zinavyokwenda ndivyo ninavyozidi kuupenda zaidi hadi najishangaa, hivyo wengine wakienda huku na kule mimi natumia muda huo kulala, ningekuwa napenda starehe nisingekuwa nacheza hadi leo hasa kwa nafasi yangu,” anasema na kuongeza;
“Nikiwa mapumziko pia sijiachii, nina programu zangu za kufanya mazoezi, kwanza sipendi kitambi ambacho wanatakiwa kuwanacho viongozi na siyo mimi mchezaji, hivyo lazima nijitunze na ndio maana mwili wangu upo vilevile miaka nenda rudi.”
Jambo lingine linalomfanya alinde kiwango chake, anatambua vijana wengi wanatamani kufikia hatua yake, hivyo anapata nguvu ya kuhakikisha hawaangushi kupigania ndoto zao, awapo uwanjani licha ya kuisaidia timu yake, anajitahidi kuonyesha ufundi utakaokuwa funzo kwao (vijana).
“Ukiwa staa unajifunza kuishi kwa ajili ya wengine na siyo ubinafsi, kama mzazi lazima niwaonyeshe nidhamu ya kazi kwa mifano, hasa vijana wanaotamani ndoto zao ziwe kubwa na kuvuka nilichokifanya mimi kwenye soka la Tanzania,” anasema.
Anasema kuna baadhi ya wachezaji wanamwambia wanapenda uchezaji wake na wengine anawaona kupitia vyombo vya habari wakisema hivyo. Nimejulikana kwa ajili ya mpira na siyo vinginevyo na nimeona vijana wengi wanafanya vizuri sana, ninachoweza kuwashauri waiishi kwenye miiko ya soka watakuwa kwenye mwendelezo wa viwango vyao kama tunavyofanya kaka zao, pia wajue kama mpira umewatambulisha hivyo wanapaswa kuuheshimu.
Anaongeza; “Wengine ninapowaita kuwaambia wanapokosea ni wasikivu na naona mabadiliko, kikubwa walitumikie soka litawaheshimu, wajue mashabiki wapo kwa ajili ya kupata burudani, hivyo ni vyema wakafanya kazi kwa bidii, kwani umarufu unakuja wenyewe na siyo wao kuutafuta, kwanza kinachotafutwa ni pesa, kujulikana bila pesa hakuna faida.”
Anaeleza hajawahi kulazimisha kujulikana na hapendi kuishi maisha ya kujikweza, hiyo ndio sababu anapomaliza majukumu yake uwanjani anarejea kuishi na jamii. Labda niwaambie kitu watu ambao wanajulikana na jamii, kazi inayokutambulisha kwao haina maana upo tofauti nao, hiyo ni kazi kama nyingine, tunapaswa kuishi na wanaotusapoti kwa heshima.
“Ndio maana hata baada ya kutoka Simba, Yanga sikuweza kuyumba kwasababu najua soka ni kazi na siyo kuvimba pindi watu wanaponifahamu kupitia karia hiyo, lazima nijue namna ya kuishi bila kutumia vibaya umarufu, nipo Geita Gold kwa sasa bado naendelea kukiwasha kama kawaida, ila ningekuwa nimelewa umarufu ningekuwa naona tabu kwenda kucheza nje ya Simba na Yanga.” Yondani amewahi kuzichezea Simba na Yanga kwa mafanikio makubwa.