Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sunzu: Chama apewe msaidizi, Mayele anga nyingine

Chama Mayeleeee.jpeg Sunzu: Chama apewe msaidizi, Mayele anga nyingine

Wed, 7 Jun 2023 Chanzo: Mwanaspoti

“Nimechagua kuishi Tanzania, Watanzania ni watu wakarimu, nimeoa Tanzania na nina watoto watatu." Ndivyo anavyoanza kusimulia, mshambuliaji wa zamani wa Simba, Mzambia Felix Sunzu.

Mshambuliaji huyo ambaye alisajiliwa Simba msimu wa 2011/12 anasema kwa sasa anaishi jijini Mwanza pamoja na mke wake Juliana Enock ambaye ni Msukuma na wamejaaliwa kupata watoto watatu, Enock, Catherine na Mo Fernandez.

“Nimechagua kuishi Mwanza na Tanzania nilikuwa na familia muda mrefu tangu nikiwa nacheza Simba kuna kipindi tulienda Malaysia tukarudi, nakaa miaka mitano naenda nyumbani Zambia kusalimia kisha narudi tena.

“Napenda kuwa hapa pia sababu ya watoto wangu nawapenda na wao wanapenda kuishi Tanzania,” anasema Sunzu

Anasema Mwanza anafanyabiashara mbalimbali na yupo mbioni kufungua duka kubwa la vifaa vya michezo.

“Nina biashara ya kuuza nguo, jezi na vifaa mbalimbali vya michezo kule kwetu Zambia nina duka kubwa unajua Stoppila (mdogo wake) anaishi China huwa ananifungia mzigo na kunitumia."

“Kwa ujumla maisha ya Tanzania ni mazuri sana, napenda chakula kinapatikana kila wakati, kuvaa una vaa unavyojisikia, kwangu maisha ni mazuri na sitamani kwenda popote hapa nimefika.

“Watanzania ni watu wazuri sana na mimi naishi nao vizuri sifuatilii habari za mtu naangalia familia yangu na biashara zangu pamoja na mke wangu,” anasema mchezaji huyo anaependa wali, maharage na kuku.

MASHABIKI WA TANZANIA

“Unajua mashabiki wa Tanzania nawakubali sana wanaufanya mpira wa Tanzania uwe juu na sisi wachezaji tunaona mpira ni furaha na unalipa.

“Wakikupenda wanakupenda, hata akikuona anakukumbatia anakuweka daraja la juu anakufurahia na hawa ndio wanafanya wachezaji waone wana deni.

“Wanawaweka wachezaji kwenye daraja la juu ukipita mtaani, bodaboda wanakusimamisha wanataka kuzungumza na wewe hii ni nzuri sana,” anasema Sunzu.

NENO KWA CHAMA

Clatous Chama ni miongoni mwa nyota ndani ya Simba waliojitengenezea ufalme wao, mashabiki wa Simba huwaambii kitu juu ya Mwamba wa Lusaka. Lakini Senzu anaeleza;

“Clatous Chama (Simba) ni mchezaji mzuri ila anatakiwa mtu wa kumsaidia apewe wa kumkabia naona nguvu zinaenda kumalizika anatakiwa kuwekewa mtu wa kukaba.

“Alikuwepo Jonas Mkude ila naye sasa hivi kama amechoka na hakuna mwingine kama Mkude, kwa kufanya hivyo watamuongezea ubora,” anasema mshambuliaji huyo.

MAYELE KAISHIKA TANZANIA

Anasema mchezaji aliyewashika mashabiki kwa sasa ni Fiston Mayele wa Yanga kutokana na uwezo mkubwa anauonesha uwanjani.

“Haelekezwi na kocha yeye anapambana, wachezaji wengi wanatakiwa kupambana kama yeye ili kufanikisha ndoto zao,”anasema Sunzu na kuongeza;

“Wachezaji wazawa wanapaswa kuongeza juhudi, hawa wa sasa hivi unaona akifika kwenye goli akipigiwa kelele anaanza kuogopa, mshambuliaji anatengenezwa ndio maana nataka kuanzisha akademi."

ALIGONGA MASHABIKI WAKAMWOKOA

Anasimulia moja ya tukio ambalo hatalisahau Tanzania ni la kumgonga mama mmoja wakati akitoka kambini akiwa Simba.

“Kuna siku nilimgonga mama mmoja Kariakoo usiku nilikuwa natoka kambini narudi nyumbani wenzangu waliondoka na basi mimi nikachelewa kutoka nilikuwa na mke wangu.

“Sasa wakati natoka kulikuwa na akina mama pembeni, bahati mbaya nikamgonga mmoja sikumuona, unajua pale kuna watu wengi.

“Wakanisimamisha watu lakini sikusimama niliogopa kupigwa walinikimbiza nilivyoona wanaweza kuvunja vioo vya gari, nikawasha taa za ndani ya gari kisha nikasimama.

“Wakaniangalia wakanitambua, wakasema huyu ni mchezaji wetu wakaniambia nenda zako, wakatoa hela wakampa yule mama niliemgonga na wakampeleka hospitali, mimi wakataka niende nikapumzike.

“Kweli walimpeleka hospitali kesho yake nikapita pale pale ikabidi niliuzie kuhusu yule mama niliemgonga na nikataka kwenda kumuona, wakasema hapana endelea na mambo yako sisi hilo jukumu tumelibeba sisi.

“Tangu tukio lile nimebaini watanzania wanaupendo wa dhati wanazipenda timu zao,” anasema mchezaji huyo wa zamani wa FC Lupopo ya Congo.

5 ZA YANGA ZAMPA UFALME

Anasema ameendelea kuishi kifalme Tanzania kutokana na kusaidia Simba kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Ynaga.

“Mimi hadi leo naheshimika sana kila nikipita wakinijua tu, bodaboda wanasimama na kunisalimia, Kariakoo wananitunza vizuri mpaka kesho hata nikienda leo pale napewa vitu bila kuomba naweza kupata simu TV na kila kitu bila hata kuomba

“Huu ndio upendo wa watanzania hawakusahau kama umewafanyia kitu nadhani hii kitu inafanya pia wachezaji wajitume,” anasema mshambuliaji huyo ambaye amewahi pia kuichezea Esperance ya Tunisia.

KUFUNGUA AKADEMI

“Nataka kufungua akademi Mwanza ili kuendeleza vipaji kwa sababu watanzania wengi wana vipaji.

“Mimi nimetokea kwenye timu za vijana hata kule kwetu Zambia nimecheza sana timu ya chini ya miaka 20 nimepata uzoefu mkubwa, nimecheza na kila Luis Suarez mwaka 2008 na Gerald Pique kwenye timu za vijana.

“Kule ndio nilikojifunza kujiamini baadae nikaenda Experance nikiwa na umri mdogo, Tanzania hili halipo lazima niwasaidie.

“Nitawakusanya kutoka kila sehemu, vijana wapo wengi sana ambao wanahitaji kuendelezwa, kuwasafisha kwenda kutafuta maisha nje ya Nchi hilo sio tatizo kwa sababu Stopilla (mdogo wake) hizo ndio shughuli zake kusafirisha wachezaji kwenda kutafuta maisha.

Anasema ukimuondoa Mbwana Sammata bado watanzania hajajua jinsi ambavyo soka linaweza kumtoa mtu kimaisha.

“Kwetu Zambia kila mtoto anataka kucheza mpira wanaona jinsi ambavyo soka linalipa hapa Tanzania lazima watu wanufaike ndio jamii ione umuhimu wa soka,”anasema.

SIMBA ILIMUONA KUPITIA YANGA

“Nilikuja Tanzania 2010 kwa mara ya kwanza nikiwa na FC Lupopo katika mechi ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika tuliwafunga tatu na Congo nikawafunga.

“Baada ya pale Simba walikuja nakumbuka alikuja Kaburu (Geofrey Nyange) na kiukweli walinipa maisha kwa sababu walinisajili kwa fedha nyingi na walinipa mshahara wa Sh 10 milioni."

“Maisha ndani ya Simba yalikuwa kama Ulaya, tulikuwa tunapewa kila kitu tena kwa wakati tulikuwa na timu nzuri ambayo ilikuwa na uwezo wa kupata matokeo popote."

“Mashahara ule na ile fedha niliweza kujenga nyumba nne nyumbani Zambia na nyingine nilijenga Mwanza ambayo naishi hadi sasa na mke wangu.

“Maisha yanaenda vizuri napata fedha kupitia kodi na zile nyumba pamoja na biashara zangu ninazoendelea kuzifanya,” anasema Sunzu.

MAISHA YA VETERANI

Anasema kutokana na kustaafu soka kwa sasa mara chache anaichezea timu ya Mwanza Veterani ili kuweka mwili vizuri.

Chanzo: Mwanaspoti