Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Sumu ya Mtibwa iko hapa

Sumu Ya Mtibwa (18).jpeg Sumu ya Mtibwa iko hapa

Sat, 28 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mtibwa Sugar ni kati ya timu bora Ligi Kuu Bara kwa miaka mingi. Ukitaka kuizungumzia utaiweka kwenye kundi lake yenyewe kutokana na mafanikio ya mapema baada ya kukwea Ligi Kuu Bara 1996.

Ni jambo la heshima kuwa na timu hiyo Ligi Kuu Bara, lakini kadiri siku zinavyokwenda Mtibwa siyo ile. Mtibwa haina ubora ule. Mtibwa haina heshima ile.

Haitishi tena. Misimu minne ya karibuni imekuwa ikiponea chupuchupu kushuka daraja. Championship inaiita kwa haraka. Ni timu ya tatu kwa mafanikio  Ligi Kuu Bara ukitoa Yanga ambayo ina makombe 29 inafuatiwa na Simba 22, timu ya tatu hapo siyo ile unayoifikiria ni Mtibwa Sugar iliyotwaa ubingwa mara mbili mfululizo 1999 na 2000, tena ikiwa na miaka michache tangu ipande daraja.

Mtibwa ina heshima yake, lakini inaanza kupotea. Kuna mengi nyuma ya kuyumba, lakini mengine yanaonekana kuwa siri yao. Msimu huu imecheza michezo sita, lakini imeanza kupigiwa debe na takwimu kuwa ipo hatarini kushuka daraja. Vuta pumzi kidogo. Rudi pale ukurasa wa pili uangalie msimamo wa ligi. Umeiona Mtibwa ilipo? Namba zake umezielewa?

KONDO NJE,

ZUBEIR NDANI

Mtibwa imempiga chini Habib Kondo na kumrudisha mtoto wake, Zubeir Katwila aliyekuwa na Ihefu SC.

Katwila anarudi baada ya kukaa nje ya timu hiyo miaka mitatu. Anarudi akiwa anakumbuka kuwa Mtibwa imecheza mechi ya mchujo (play off) misimu miwili ya karibuni na kuponea chupuchupu. Kila kitu kuhusu timu hii anakifahamu. Ndiyo sehemu aliyocheza kwa mafanikio makubwa na kupata heshima aliyonayo sasa.

Amerudi na leseni A ya ukocha CAF. Anakwenda akiwa ameshaiadhibu Yanga mara mbili akiwa na Ihefu, lakini anarudi na changamoto ya kukaa mbali ya timu hiyo kwa miaka mitatu.

Katwila ni mtoto wa nyumbani pale Mtibwa walewale ambao imekuwa ikiwataka muda wowote wanarudi sehemu ambayo makocha wageni wamekuwa wakihaha kupata matokeo lakini wakirudi wanafanya vizuri.

Mecky Maxime, ni mtoto mwingine wa nyumbani anayependwa sana hapa mwishoni wakati anaondoka mambo yalikuwa magumu, lakini msimu huu kazi yake inamtofautisha na familia, katika michezo minne ambayo Mtibwa imepoteza mmoja ni dhidi ya Kagera ambayo inafundishwa na Mecky, tena walifungwa palepale Manungu huku kocha huyo akionekana kuhaha kwenye benchi kuhakikisha timu yake inapata mabao mengi zaidi ya 2-0 iliyokuwa inaongoza.

Nani anakumbuka msimu mmoja nyuma wakati timu imebakiza michezo mitatu ishuke? Timu iliyokuwa chini ya Salum Mayanga ambaye ni mtoto mkubwa wa nyumbani, huwa anaondoka na kurudi, lakini dakika za mwisho ikaonekana mambo ni magumu  zikiwa zimebaki mechi tatu, akakabidhiwa Awadhi Juma ainusuru. Jambo la kufurahisha ni kwamba Juma alicheza Mtibwa na hapa ni nyumbani kwake. Walikuwa wanaonekana watoto wote wa nyumbani jukwaani wakati Mtibwa wakicheza mechi tatu za mwisho, walionekana Mecky, Katwila, Henry Joseph, Vincent Barnabas, Shaabani Nditi na wengine wengi kuonyesha ni familia.

Kama walisaidiana mazoezini sijui, lakini kama ni ushauri nafahamu walishauriana kwa simu na vikao mbalimbali kuhakikisha timu inabaki Ligi Kuu, jambo zuri walishinda michezo miwili kati ya mitatu na kucheza ‘play off’ ambayo iliwabakiza kwenye ligi kama msimu mmoja nyuma.

SWALI MUHIMU

Kwanini wanapitia maisha haya wakati inaonekana ni timu ambayo inafuata misingi sahihi ya kukuza soka. Wanatengeneza makocha bora. Wana uwanja wa soka mzuri tu hawalii shida mara kwa mara. Ukiwatazama Mtibwa utagundua maisha yalianza kuwa magumu kuanzia msimu wa 2019/2020. Msimu huo Mtibwa walianza kuyumba na kumaliza  wakiwa nafasi ya 14 na pointi 45, wakati timu zikicheza michezo 38 kwa msimu, zikiwa 20.

Lakini msimu uliofuata  iliendelea kuyumba baada ya kumaliza ligi nafasi ya 14 tena, sasa ikiwa imeshuka baada ya kukusanya pointi 39, 2021/2022 hali iliendelea kuwa mbaya, walimaliza msimu wakiwa na pointi 31, lakini wakiwa nafasi ya 13.

2022/2023, hapa walionekana kama wameamka na kushika nafasi ya 10 na pointi 35, lakini msimu huu wanaonekana kurudi nyuma baada ya kuanza vibaya na sasa hawaonekani kama wanaweza kuamka.

MASWALI MENGI

Kwenye karatasi hii ni timu bora, ina wachezaji wengi wa zamani kila msimu kwenye benchi, wenye uchungu haswa, lakini wanaonekana kushindwa kushauri kuhusu mwendelezo wa timu.

Hawa kina Mecky, Zubeir, Nditi, Joseph, Mayanga na wengine linapokuja suala la timu kuuza hawawaambii ukweli mabosi. Ama wanaogopa au wanaamini soka ni mchezo rahisi. Ukitazama kwenye Ligi Kuu Bara, Mtibwa wana mastaa wengi, lakini walivyoondoka hakukuwa na mbadala aliyesajiliwa, watazame wachezaji kama Abuutwalib Mshery, Bakari Majogolo, Mzamiru Yassin, Dickson Job, Kibwana Shomary na Dickson Kibabage. Hawa ni watoto haswa wa nyumbani wakifika pale wana heshima, lakini waliuzwa bila mbadala sahihi na sehemu waliyopo wanafanya makubwa kila siku imebaki sifa tu walianzia Mtibwa.

Mfano msimu uliopita ambao Mtibwa walimaliza nafasi ya kumi, walisahau kuwa nyuma waliponea chupuchupu na kuuza mastaa kama David Kameta ‘Duchu’ (Simba), Nassor Kiziwa, Ismail Mhesa, Onesmo Mayaya, Athuman Masumbuko ‘Makambo’ (Mashujaa), Charles Ilanfya, Issa Rashid ‘Baba ‘Ubaya’, Vedastus Mwihambi (Ihefu), Cassian Ponera, Pascal Kitenge, Balama Mapinduzi (Coastal Union) na James Kotei. Hawa asilimia 90, walipokwenda ni mastaa wakubwa wachache ndiyo wamechuja na wanazisaidia timu kufanya kweli kwenye ligi. Tazama wale waliokwenda Ihefu alipokuwa mtoto wa nyumbani Zubeir.

Lakini ajabu, mbadala wa wachezaji hao wengi wameonekana kufeli Mtibwa, baada ya kuuza walisajili kundi kubwa mwishoni, Kelvin Nashon, Yassin Mustapha (Singida Fountain Gate), Matheo Anthony, Abdul Hillary (KMC), Seif Karihe (Dodoma Jiji), Juma Liuzio, Haruna Shamte (Geita Gold), Mohamed Kassim (JKT Tanzania), Kassim Haruna (Namungo FC), Fredrick Magata (Mbeya Kwanza), Awadh Salum Juma (Mbeya City) wote hawaonekana kuwa wachezaji wa Mtibwa na labda kiwango cha kuuza na kununua vilikuwa havilingani hata kidogo.

TIMU YA VIJANA

Kwenye hii wamefanikiwa asilimia 100. Kama ni kweli kuwa na timu bora kunaanzia kwa vijana, kwanini Mtibwa wanafeli? Wana timu bora ya vijana ambayo imetwaa ubingwa mara tano mfululizo.  Swali linarudi kulekule juu baada ya kufanya vizuri huenda wapi? Ni kweli kuwa Mtibwa hawaikatai fedha ikienda mezani kwa mabosi wanaichukua kirahisi sana na kumwachia yeyote? Nani anamkumbuka Makambo ambaye alikuwa mfungaji bora wa timu ya vijana U 20 msimu uliopita, kila mtu alisema lake, lakini mwishoni alikwenda Mashujaa.

Ni kweli kwamba hawa makocha ambao ni watoto wa nyumbani wanashindwa kushauri haya? Kama Mtibwa wanatwaa ubingwa miaka mitano hao wanaokuwa bora ambao tumekuwa tukiwaona Uwanja wa Chamazi wanakwenda wapi.

Nafikiri kama hawa makocha wanaozalishwa na Mtibwa hawatakuwa wakweli kuhakikisha wanainusuru timu ya tatu kwa mafanikio kwenye Ligi Kuu Bara, watakwenda Championship bila maswali. 

Tupe maoni yako. Wewe unadhani ni nini tatizo la Mtibwa kwenye miaka ya hivikaribuni? Niandikie ujumbe 0658- 376 417

Chanzo: www.tanzaniaweb.live