Staa wa zamani wa Liverpool, Daniel Sturridge amesema ana uhakika mkubwa miamba hiyo ya Anfield haitakuwa kwenye wakati mgumu eti kwa sababu tu Jurgen Klopp ameachana na kikosi hicho.
Klopp aliachana na Liverpool mwishoni mwa msimu baada ya miaka tisa na kibarua hicho cha kuinoa miamba hiyo ya Anfield kimekuja kuchukuliwa na Arne Slot, aliyenaswa kutoka Feyenoord.
Liverpool imefanya mabadiliko kadhaa pia kwenye ngazi za juu, ambapo Michael Edwards na Julian Ward walirejea kwenye timu na Richard Hughes ametua akitokea Bournemouth kuja kuwa mkurugenzi mpya wa michezo.
Na Sturridge ana uhakika kwa uongozi wa Edwards na Mike Gordon, ulianza kwa kufanya jambo sahihi katika uteuzi wa kocha Slot.
Fowadi huyo wa zamani wa England alisema: “Klopp alifanya vitu vikubwa sana. Lakini, sasa klabu ipo kwenye kipindi cha mpito. Kutakuwa na kocha mpya na wachezaji wengine mikataba yao itakwisha ” ni suala la muda tu. Sioni kama Liverpool itatikisika.”
Staa wa Liverpool, Cody Gakpo, ambaye aliwahi kucheza dhidi ya Feyernoord ya Slot na AZ Alkmaar kipindi alipokuwa PSV Eindhoven, anaamini staili ya soka la Mdachi huyo inaendana kabisa na Liverpool.