Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Stumai ufundi, kipaji vinambeba kila kona

Stumai Abdallah Stumai ufundi, kipaji vinambeba kila kona

Mon, 18 Dec 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Licha ya mastaa wengi wanaocheza Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) kubadili mwonekano wao baadhi wakijiweka kama wanaume lakini ni tofauti kwa Stumai Abdallah.

Staa huyo ambaye anamudu kucheza nafasi nyingi uwanjani ameliambia Mwanaspoti yeye ni mwanamke na kila mwanamke ana ndoto ya kuolewa, hivyo anaamini muda ukifika atakuwa mke na mama.

WATOTO WANNE FRESHI

Suala la kuzaa ni mipango ya Mungu lakini kila mwanamke amekuwa na mipango yake kwenye suala la uzazi kuna ambao wanatamani mtoto mmoja, watatu na wengine idadi kubwa zaidi kama ilivyo kwa kiraka wa JKT Queens ambaye amekiri anamani kuwa na watoto wanne.

“Mimi ni mwanamke licha ya kucheza soka lakini nina ndoto ya kuolewa na baadae kuwa mzazi wa familia ya watoto wa kike wawili na wa kiume wawili wakipungua basi ni watoto watatu,” anasema.

KUVUNJA REKODI YAKE

Msimu ulioisha akiwa miongoni mwa wachezaji waliovuja jasho timu yao kutwaa taji la ligi kiraka huyo alifunga mabao 13 ametamba kuvunja rekodi yake msimu huu.

“Malengo yangu msimu huu ni kuvunja rekodi yangu na ikiwezekana niweze kutwaa kiatu cha dhahabu mwishoni mwa msimu;

“Sio rahisi lakini lolote linawezekana kutokana na malengo na upambanaji wangu ikiwa ni pamoja na kuhakikisha naisaidia timu yangu kutetea taji la ligi.”

PRECIOUS ANA GUU LA DHAHABU

Ni nadra kwa wachezaji kukubali uwezo wa wachezaji wengine kutokana na kuamini katika vipaji vyao kwa kila mmoja lakini hii ni tofauti kwa Stumai ambaye amemtaja mshambuliaji wa Yanga Precious Christopher kuwa ni mchezaji mwenye guu la dhahabu.

“Ligi ya Wanawake ina wachezaji wengi wanaotumia miguu ya kushoto lakini kwangu Precious ni mchezaji bora kwa wanaotumia mguu huo.

“Anajua kuutumia mguu wake wa kushoto vizuri ndiye mchezaji wangu bora kwa wachezaji wa kike,” anasema.

KISA SOKA APANDA NDEGE

Suala la kupanda ndege licha ya wengi kutokuwa la kawaida kwao kama alivyothibitisha kiraka wa JKT Queens kuwa alianza kwa uoga na sasa ni kawaida.

“Kwanza kupanda ndege ilikuwa ni moja ya ndoto yangu kuwa ipo siku nitapanda nashukuru Mungu mpira umetimiza ndoto hiyo japo haikuwa rahisi.

“Nilianza kwa uoga lakini sasa ni kawaida kwani nimepanda mara nyingi na nina furaha kwani nimetimiza ndoto yangu ya kuwa miongoni mwa watu waliowahi kupanda ndege,” anasema

KUMBE MWANDISHI

Licha ya kuwa bora katika kusakata kabumbu na kumudu nafasi nyingi uwanjani fundi huyo amethibitisha kama sio soka basi ndoto yake ilikuwa ni kuwa mwandishi wa habari.

“Mimi nje ya mpira nilikuwa napenda zaidi taaluma ya uandishi wa habari kama ilivyo wewe lakini kipaji changu cha soka ambacho kiligunduliwa na wazazi wangu kikachukua kipaumbele.

“Sikumbuki nilianza kucheza soka nikiwa na umri gani, ila nilijitambua zaidi nikiwa darasa la saba, hivyo soka likachukua nafasi kubwa kuliko mambo ya shule lakini hata ikatokea nikaacha soka nitatimiza lengo langu na kuwa mwanahabari,” anasema.

AITAJA SIMBA, TUZO

Baada ya kupoteza taji la Ngao ya Jamii dhidi ya Simba kwa mikwaju ya penalti 5-4 baada ya dakika 90 kutoana jasho kwa sare ya bao 1-1, Stumai anasema haikuwa bahati yao kwani waliwazidi Simba kila eneo.

“Haikuwa bahati yetu ilikuwa upande wa Simba kwenye kucheza hawakutuzidi ila kwakuwa penalti hazina mwenyewe wakatuwini eneo hilo baada ya sisi kushindwa kuumaliza mchezo ndani ya dakika 90 licha ya kuwa bora,” anasema.

Stumai aliondoka na tuzo mbili akiwa mfungaji bora wa mashindano akifunga mabao mawili moja kwenye fainali na lingine nusu fainali dhidi ya Singida Fountaine Gate Princess na tuzo nyingine ilikuwa ni ya mchezaji bora wa fainali.

“Kujituma na kufuata maelekezo ya kocha ndio siri ya mafanikio. Kwenye suala la kutwaa tuzo mbili na naamini nimeanza vizuri natarajia tuzo nyingine zaidi msimu huu ambao ligi inatarajia kuanza Desemba 22.”

NI KIRAKA

Erasto Nyoni wa Namungo anatajwa kuwa ni mchezaji anayemudu nafasi nyingi kwenye soka la wanaume. Kwenye soka la wanawake anatajwa Stumai.

“Nacheza nafasi zote tena kwa ufasaha isipokuwa eneo la kipa, msimu uliopita nimetumika eneo la ushambuliaji, beki zote mbili kushoto na kulia na winga zote nimecheza kwa usahihi;

“Kocha ndiye anayeamua nicheze wapi, nafurahia hilo kwani linanipa nafasi ya kutumika kikosini tofauti na mchezaji ambaye anacheza nafasi moja. Ni ngumu kukosa nafasi kabisa kwani nazimudu zote,” anasema kiraka huyo ambaye amethibitisha kuwahi kutamani kuacha soka kutokana na changamoto za mchezo huo ambazo hakutaka kuziweka wazi.

Chanzo: Mwanaspoti