Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Straika la mabao latua Mashujaa

Karihe Pic Data Straika la mabao latua Mashujaa

Thu, 27 Jun 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Klabu ya Mashujaa ya mkoani Kigoma imekamilisha usajili wa aliyekuwa mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Seif Rashid Karihe kwa mkataba wa mwaka mmoja huku kukiwa na kipengele cha kuongeza mwingine endapo watavutiwa na uwezo wake.

Msimu uliopita, licha ya Mtibwa kushuka daraja baada ya mwenendo mbaya, nyota huyo alionyesha uwezo mkubwa na kufunga mabao saba na kuasisti moja katika Ligi Kuu Bara akiibuka kinara ndani ya kikosi hicho cha Walima Miwa wa Manungu.

Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo zililiambia Mwananchi kwamba baada ya Mtibwa kushuka ilianza kuwasiliana na mchezaji huyo mapema ili kuinasa saini yake ikiamini atakuwa ni mbadala sahihi wa Adam Adam aliyeondoka na kujiunga na Azam FC.

"Ni kweli Karihe tumepata saini yake na tunaendelea na usajili wa nyota wengine na tutakapokamilisha tutaweka wazi kwa wote tutakaowasajili na kuwaacha, ni mchezaji mzuri ambaye amependekezwa na benchi la ufundi," alisema kiongozi mmoja.

Kwa upande wa Meneja wa Mashujaa, Athumani Amiri alipotafutwa kuzungumzia suala hilo alisema, ni mapema sana kuweka wazi silaha walizozisajili ila muda ukifika wataweka wazi kila kitu kwa sababu yapo mambo ambayo viongozi wanaendelea nayo.

"Kuhusu usajili huu ni wakati wake na siwezi kuzungumza kwa sababu yapo mambo mengine ambayo viongozi hawajayakamilisha hivyo yatakapokuwa sawa tutawatangazia mashabiki zetu, kikubwa wajue tumesajili wachezaji bora na wenye uwezo mkubwa."

Amiri aliongeza, kikosi hicho kinatarajia kuingia kambini kuanzia Julai Mosi mwaka huu ili kuanza maandalizi ya msimu ambapo kitakusanyika mkoani Kigoma kwa siku kadhaa kisha baada ya hapo kitakwenda visiwani Zanzibar.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live