Baada ya straika Yusuph Athuman kukosa namba Yanga, anaamini atafanya makubwa katika timu yake mpya ya Coastal Union, akiamini mzunguko wa pili atakuwa na rekodi ya kukumbukwa.
Yanga imemtoa kwa mkopo Athuman, baada ya nafasi finyu ya kupenya kikosi cha kwanza mbele ya Fiston Mayele,tofauti na wenzake kama Chrispin Ngush kabla hajapata majeraha angalau alikuwa anapata nafasi, huku Clement Mzinza akionekana kuaminiwa na sasa ana mabao mawili.
Kwa mara ya kwanza baada ya kutua Coastal Union, Athuman aliliambiwa Mwanaspoti kwamba ni fursa kwake kupambana na kuonyesha uwezo ili kurejesha makali yake ya kucheka na nyavu.
"Kujiunga na Coastal Union kwangu ni fursa ya kujijenga kiuwezo na kujiamini zaidi, ukitofautisha na Yanga ambako kulikuwa na ushindani mkali zaidi wa namba.
"Sina maana kwamba Coastal Union nitacheza kwa mtelemko, bali natakiwa kupambana kwa kadri nitakavyoweza ili kuhakikisha narejea kwenye kiwango cha juu cha kufunga mabao."
Alisema anaamini ana vitu vingi vya kuvifanyia kazi ndani ya kikosi cha Coastal Union ambavyo vitamfanya kipaji chake kizidi kuchanua na kuwa mchezaji mwenye thamani kubwa.
"Haijalishi una kipaji cha aina gani, unapokosa nafasi ya kucheza kinakuwa hakina maana, lazima uwe unakifanyia kazi ndipo unaweza ukaona thamani yake kubwa, hivyo naamini ni wakati wangu wa kupambana," alisema.