Mshambuliaji Moses Phiri aliyetangazwa kutemwa Simba katika dirisha dogo ili kupisha mastaa wapya wa kigeni kutua Msimbazi, ameibukia Power Dynamos ya Zambia akijiunga nayo kwa mkopo wa miezi sita hadi mwisho wa msimu huu.
Nyota huyo ameondoka Simba kutokana na kilichoelezwa kutokuwa kwenye kiwango kizuri akiungana na mastaa wengine wakiwemo, Nassoro Kapama, Jimmyson Mwanuke, Shaaban Idd Chilunda, Hamis Abdallah, Mohamed Mussa na Jean Baleke.
Phiri aliyejiunga na Simba, Juni 15, 2022 akitokea Zanaco pia ya Zambia na katika msimu wa kwanza alikuwa katika kiwango bora akifunga mabao 10 katika mechi za nusu msimu za Ligi Kuu kabla ya kuumia na kuibukia msimu huu ambapo hadi anaondoka alikuwa amefunga mabao matatu tu.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Buildcon kabla ya kutua Simba akiwa na Zanaco alifunga jumla ya mabao 14 katika Ligi Kuu ya Zambia akishika nafasi ya pili nyuma ya mfungaji bora kwa msimu huo, Ricky Banda aliyemaliza akiwa kinara na mabao 16.
Msimu wa 2020/2021 ulikuwa bora kwa nyota huyo wakati akiichezea Zanaco ambapo alikuwa mfungaji bora wa Ligi ya Zambia kwani alimaliza na jumla ya mabao 17 na kukiwezesha kikosi hicho kufuzu moja kwa moja Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Mzambia huyo mbali na kutamba kwenye Ligi Kuu Bara kabla ya mambo kumbadilikia msimu huu, pia aliisaidia Simba kwenye harakati za kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita na timu hiyo kwenda kutolewa robo fainali.
Phiri aliifungia Simba matatu wakati wakiing'oa Big Bullets ya Malawi kwa jumla ya mabao 4-0, akifunga mawili kwenye ushinfi wa ugenini wa mabao 2-0, kisha kuongeza moja walipoizamisha jijini Dar es Salaam pia kwa mabao 2-0, lingine likifungwa na John Bocco.