Mshambuliaji wa Power Dynamos, Joshua Budo amekiri kuwa mchezo wao dhidi ya Simba SC Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa katika uwanja wa Levy Mwanawasa Zambia Septemba 16 utakuwa mgumu.
Akizungumza na Mwanaspoti Budo amesema ugumu wa mchezo huo unatokana na mechi kujumuisha mambo mengi ya fedha na hatima ya baadhi ya wachezaji kutamani kutoka nje ya Zambia.
"Mchezo wetu utakuwa mgumu kwasababu tunapambania kuhusu jambo fulani, huku kuna pesa na pia tunatumia michezo hii kwa ajili ya sisi kujitangaza kimataifa tofauti kabisa na mchezo ule wa kirafiki tuliocheza nao wa Simba Day ile ilikuwa burudani tu hata kupoteza mchezo haikutuuma sana"
Ameongeza kuwa wanatambua Simba ni timu kubwa Afrika na timu yenye wachezaji wenye majina makubwa ila walichopanga ni kumaliza mchezo mjini Ndola kwa ushindi wa mabao 3-0.
"Tunajua Simba ni timu kubwa na watataka kuthibitisha hilo kuanzia kwetu ili wafuzu kwenye makundi, inawachezaji wenye majina makubwa, tumepanga kumaliza mchezo nyumbani kwa ushindi wa mabao 3-0,"
"Natamani kufunga dhidi ya Simba kwasababu hii ni timu kubwa na pia haya ni mashindano makubwa, nilishindwa kufunga siku ya Simba Day lakini kwenye mchezo ujao lazima nifunge"
Budo msimu uliopita alimaliza kwa kufunga mabao saba na kuwa mshambuliaji namba mbili katika timu hiyo.