Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Straika, Mabeki dili Tabora United

Tabora United Wafungiwa FIFA.jpeg Kikosi cha Tabora United

Thu, 16 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Tabora United inaendelea kujifua kwa ajili ya mechi za zijazo za Ligi Kuu Bara, huku kocha Goran Kopunovic amesema endapo ataingia kwenye usajili wa dirisha dogo basi atakwenda kutafuta washambuliaji wenye makali ya kufunga mabao na mabeki.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kopunovic alisema changamoto kubwa ya kiufundi anayokabiliana nayo akiwa Tabora United ni kutokuwa na washambuliaji bora wa kumalizia nafasi ambazo wanatengeneza uwanjani.

Kopunovic alisema mipango yake ya muda mfupi ni kuendelea kuwaongezea makali washambuliaji alionao sasa kwenye kikosi hicho, huku ile ya muda mrefu ni kuanza kutafuta washambuliaji na mabeki walio bora.

Kwenye mechi zake 9 walizocheza Tabora wamejikuta wakipata sare ya bila mabao kwenye mechi tano dhidi ya Singida Big Stars, Coastal Union, KMC na Kagera Sugar.

Timu hiyo imeshinda mechi mbili dhidi ya Tanzania Prisons na Dodoma Jiji huku wakipoteza mbili mbele ya Azam FC na JKT Tanzania wakiwa kwenye nafasi ya 7 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

“Tunakabiliwa na changamoto ya kufunga mabao, tumefanikiwa kufunga lakini sio kwa kiwango ambacho kinatakiwa kulingana na nafasi ambazo tunatengeneza,” alisema Kopunovic.

“Tutaendelea kulifanyia kazi lakini muda ukifika tutaangalia namna nzuri ya kuleta watu bora zaidi ambao watakuja kutuongezea upande wa kiungo mkabaji, kiungo mshambuliaji na beki wa kulia ili tuwe na nguvu.”

Kwenye mechi hizo tisa, Tabora imefanikiwa kufunga mabao matano huku ikiruhusu mabao 7 ikiwa ndio msimu wake wa kwanza kwenye ligi tangu ipande msimu huu.

“Kuna maboresho tutalazimika kuyafanya tutahitaji watu wa kuja kutuongezea nguvu wenye ubora, nafurahia kazi inayoendelea kuonyeshwa na vijana tulionao, wanafanya kazi kubwa lakini tutahitaji ziadi kwa siku za hivi karibuni,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live