Straika wa Azam FC, Abdul Sopu ataukosa mchezo wa ligi kuu dhidi ya KMC kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya mguu.
Mchezo huo wa ligi unatarajiwa kupigwa Oktoba 22 mwaka huu kwenye Uwanja wa Uhuru, Jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia maandalizi ya timu yao, Ofisa Habari wa muda wa Azam FC, Hasheem Ibwe amesema kikosi chao tayari kimeanza maandalizi ya kujiandaa na mchezo huo ujao.
“Kikosi tayari kimeanza maandalizi ya mchezo ujao wa ligi dhidi ya KMC ambapo tutakuwa ugenini na macho yetu na masikio yanauangalia mchezo huo muhimu kwetu.
“Tutawakosa nyota wetu wawili wenye majeraha ambao ni Abdul Sopu na Pape Maliku ambaye yeye tayari ameanza mazoezi mepesi.
“Sopu alipata majeraha ya mguu na hivi sasa yupo kwenye hospitali moja hapa Dar kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi ili kugundua ukubwa wa jeraha lake hivyo tutamkosa kwenye mchezo ujao.”